Rais Samia Suluhu Hassan ametoa ahadi ya kuendelea kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa utawala bora unapatikana nchini Tanzania.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam, mara baada ya kupokea ripoti kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Rais Samia alisema kuwa ukaguzi uliofanywa na CAG unaonyesha matokeo mazuri ya juhudi za serikali katika kuimarisha taasisi za umma.
"Taasisi hizi mbili, CAG na Takukuru, zitaendelea kufanya kazi kwa uadilifu na uzalendo mkubwa kwa manufaa ya taifa letu. Sisi, upande wa serikali, tuko tayari kufanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti hizo," alisema Rais Samia.
Alieleza kuwa serikali inafanya jitihada kubwa kuhakikisha kuwa taasisi za umma zinaimarishwa ili ziweze kutumia rasilimali za umma kwa ufanisi zaidi. Rais Samia alionyesha kufurahishwa na matokeo ya ukaguzi, ambayo yanaonyesha kuongezeka kwa ufanisi katika matumizi ya rasilimali za serikali.
"Pamoja na mapungufu yaliyotajwa na CAG, mengi ni ya kipindi cha nyuma, lakini kwa ujumla, kumekuwa na ufanisi mkubwa katika matumizi ya rasilimali za serikali. Hii ni faraja yetu kama serikali, kwani inaonyesha tumeweza kukuza uwazi, uwajibikaji, na kuleta utawala bora," alifafanua Rais Samia.
Alisema ripoti ya Takukuru inaonyesha kuongezeka kwa ufanisi ndani ya taasisi hiyo na katika taasisi za umma kwa ujumla. Alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya rushwa, jambo ambalo ni ishara nzuri ya mafanikio ndani ya taasisi za umma.
Rais Samia aliahidi kuwa serikali itafuatilia kwa karibu mjadala wa bunge kuhusu ripoti ya CAG na itafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na Takukuru ili kuimarisha utawala bora nchini.
Alisema matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na mifumo ndani ya taasisi za umma yamesaidia kupunguza kasoro zilizokuwa zikijitokeza hapo awali.
"Takukuru wametuambia kuna kiwango kikubwa cha kukuza ufahamu na kujenga ujasiri kwa wananchi wa Tanzania kufahamu rushwa ni nini na kujenga ujasiri wa kuisema," aliongeza.
Alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu kuhusu rushwa kwa vijana kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu, akisema hatua hiyo itasaidia kujenga kizazi chenye utamaduni wa kupinga rushwa.
Rais Samia aliipongeza Ofisi ya CAG kwa kazi nzuri wanayofanya, ikiwa ni pamoja na kuchunguza ufanisi wa miradi mbalimbali na mifumo ya TEHAMA katika taasisi za umma.
Alimuomba Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, kupokea ripoti hizo na kuziwasilisha bungeni ili zifanyiwe kazi kwa wakati. Serikali imeahidi kuzipitia ripoti hizo kwa makini na kuchukua hatua stahiki.