Rais Samia Aelekeza Bilioni 45 Kutatua Tatizo la Maji Dodoma, Miradi Minne Yaanza Kutekelezwa

economy | Wed Apr 16 2025


Rais Samia Aelekeza Bilioni 45 Kutatua Tatizo la Maji Dodoma, Miradi Minne Yaanza Kutekelezwa

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ametangaza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza utekelezaji wa miradi ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni 45, lengo likiwa ni kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi katika jiji la Dodoma. Miradi hii minne inatekelezwa kwa haraka ili kuboresha huduma za maji jijini humo, wakati mipango ya miradi mikubwa zaidi, kama vile mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria na Bwawa la Farkwa, ikiendelea kufanyiwa maandalizi.


Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba wa awamu ya pili ya Mradi wa Nzuguni kati ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) na mkandarasi Bahaji Construction, ambao una thamani ya shilingi bilioni 5.6 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 15, Waziri Aweso alisema, “Mbunge wenu (Anthony Mavunde) alileta maombi kwa Mheshimiwa Rais Samia kuhusu uchimbaji wa visima virefu alipozungumza na wananchi pale Mpunguzi. Wizara yetu ilipokea maelekezo na tumeyafanyia kazi baada ya Rais kutoa fedha kwa ajili ya miradi hii minne, ambayo inalenga kuboresha huduma za maji safi Dodoma wakati tunasubiri miradi ya Ziwa Victoria na Farkwa.”


Miradi mingine iliyotajwa na Waziri Aweso, pamoja na mradi wa usambazaji maji wa visima vya Nzuguni, ni pamoja na Mradi wa Maji wa Nala wenye thamani ya shilingi bilioni 3.8, Mradi wa Maji wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wenye thamani ya shilingi bilioni 1.2, na Mradi wa Maji katika Mji wa Serikali wenye thamani ya shilingi bilioni 35.6.


Aidha, Waziri Aweso alieleza kuwa Wizara ya Maji, kwa kushirikiana na DUWASA na RUWASA, imeunda timu zinazoendelea na utafiti wa maji chini ya ardhi na uchimbaji wa visima katika maeneo ya Mzakwe, Nzuguni, Kisasa, Nkuhungu, Miganga, Zuzu, Msalato, na Ihumwa. DUWASA pia inaendelea na taratibu za manunuzi kwa ajili ya mradi wa maji safi kwa maeneo ya Elishadai, Ihumwa, na Mahomanyika, ambayo yanatarajiwa kuhudumiwa na chanzo cha maji cha Nzuguni.


Waziri Aweso alimuagiza mkandarasi kutekeleza mradi wa Nzuguni ndani ya miezi 7 badala ya 15 kama ilivyoainishwa kwenye mkataba, akisisitiza kuwa wizara haitakuwa kikwazo katika utekelezaji wa miradi ya maji Dodoma. “Mkataba unaonyesha mradi utakamilika ndani ya miezi 15, lakini mimi nimefanya kazi katika sekta hii kwa takriban miaka nane au tisa. Mradi huu haupaswi kuchukua miezi 15; unapaswa kukamilika ndani ya miezi sita au saba. Tunapaswa kuharakisha ili wananchi wanufaike na uwekezaji huu wa Rais Samia,” alisema.


Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema kuwa utekelezaji wa mradi wa usambazaji maji kupitia Nzuguni utasaidia kupunguza tatizo la mgao wa maji kwa wananchi wa maeneo ya Nkuhungu, Miganga, Chidachi, Nzuguni, Kisasa-Bwawani, Mwangaza, Ipagala, Ilazo, Swaswa, Mpamaa, na Njedengwa.


Mkurugenzi wa DUWASA, Aron Joseph, alisema kuwa mradi huo utahusisha kuongeza ukubwa wa mabomba ya usambazaji maji, ambayo yatawezesha kusambaza maji kwa wastani wa lita milioni 20 kwa siku. “Eneo la Nzuguni lina visima tisa vilivyokamilika, vyenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 20 kwa siku. Kwa sasa, visima vitano vyenye wastani wa lita milioni 10 ndivyo vinavyotumika. Mradi huu utawezesha visima vingine vinne kuingizwa kwenye mfumo wa usambazaji, hivyo kuongeza upatikanaji wa maji,” alisema.


Aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 81 hadi 91 kwa siku, sawa na ongezeko la asilimia 30 kutoka chanzo cha Nzuguni, na kuwahudumia watu wapatao 123,095. Pia, kutaleta unafuu wa upatikanaji wa maji katika maeneo ya Nkuhungu, Miganga, Mkonze, Chidachi, na Makulu Ostabeyi. “DUWASA inaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Maji kwa kuendelea kuipa kipaumbele Dodoma, hasa DUWASA, katika kutatua changamoto za upatikanaji wa maji safi,” alihitimisha.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.