Waziri wa Maji, Juma Aweso, ametoa agizo kali kwa Mamlaka zote za Maji Safi na Usafi wa Mazingira nchini, akizipiga marufuku kukata huduma ya maji kwa wateja wanaodaiwa madeni wakati wa mwisho wa wiki na siku za sikukuu.
Agizo hili lilitolewa hivi karibuni wakati Waziri Aweso alipokuwa katika ziara ya kikazi kukagua miradi muhimu ya uchimbaji visima vya maji katika jiji la Dodoma, pamoja na mradi mkubwa wa kimkakati wa maji wa miji 28 uliopo wilayani Chamwino, mkoani Dodoma.
Waziri Aweso alisisitiza kuwa ni kinyume cha utaratibu na ni marufuku kwa watumishi wa wizara hiyo kusitisha huduma ya maji kwa wateja wanaodaiwa ankara za maji wakati wa mwisho wa wiki na sikukuu. Alieleza kuwa hatua hiyo inawaathiri wananchi wakati wanapumzika na familia zao.
"Watumishi wa Wizara ya Maji ni marufuku kumkatia maji mtu siku ya 'weekend' au sikukuu. Unakuta watu wamepumzika na familia zao, mara huduma ya maji inakatwa. Hii ni marufuku kuanzia sasa, na haya ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan," alisema Waziri Aweso kwa msisitizo.
Sambamba na agizo hilo, Waziri Aweso alitoa maelekezo kwa mkandarasi Megha Engineering, anayetekeleza mradi wa maji wa miji 28 wilayani Chamwino, kuharakisha kazi na kufanya kazi hata usiku ili kukamilisha mradi huo kwa wakati. Alieleza kuwa fedha za mradi huo tayari zimetolewa, na kwa mujibu wa mkataba, mkandarasi alipaswa kuwa amefikia asilimia 70 ya utekelezaji, lakini hadi sasa yupo katika asilimia 15 tu.
"Mradi huu fedha tayari zimetolewa, na kwa mujibu wa mkataba, hadi sasa mkandarasi alipaswa kuwa amefika asilimia 70 ya utekelezaji, lakini yupo asilimia 15. Kwa hiyo, anapaswa kufanya kazi usiku na mchana ili kufikia matakwa ya mkataba. Msimamizi wa mradi unapaswa kumsimamia, vinginevyo nitakuondoa wewe," alionya Waziri Aweso.
Mbunge wa Chamwino na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, alishukuru serikali kwa kutekeleza mradi huo, akisema utasaidia kumaliza tatizo la mgawo wa maji katika wilaya hiyo. Hata hivyo, alieleza kuwa mahitaji ya maji kwa siku katika wilaya hiyo ni lita milioni 7.5, wakati uzalishaji ni lita milioni 4.8, hivyo kuna upungufu wa lita milioni 2.7.