Serikali ya Tanzania, kupitia Wizara ya Nishati, imewakutanisha wadau muhimu ili kupata maoni yao kuhusu ramani mpya ya miaka 25 itakayoongoza matumizi ya rasilimali ya gesi asilia nchini. Mpango huu kabambe, unaojulikana kama NGUMP (National Gas Utilization Master Plan), unalenga kuleta mapinduzi katika sekta ya nishati na kukuza uchumi kwa kiwango kikubwa.
Akifungua warsha hiyo jijini Dar es Salaam leo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. James Mataragio, alieleza kuwa mpango huu utawezesha serikali kufahamu kwa uhakika mahitaji halisi ya gesi katika maeneo manne makuu: uzalishaji wa umeme, viwanda, usafirishaji (CNG), na matumizi ya majumbani kwa ajili ya kupikia. Hii itasaidia katika upangaji bora wa miundombinu na ugawaji wa rasilimali hiyo adhimu.
"Kwa muda mrefu tumekuwa tukitumia gesi, lakini sasa tunataka kuwa na dira inayoeleweka itakayotuongoza kwa miaka 25 ijayo. Mpango huu wa NGUMP utatuwezesha kujua kila sekta inahitaji kiasi gani cha gesi, na hivyo kurahisisha ujenzi wa miundombinu na utafutaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi," alisema Dk. Mataragio.
Mpango huu, unaoandaliwa kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa mikakati mikubwa ya kitaifa. Unategemewa kuwa nguzo katika kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ambapo sekta ya nishati imetajwa kama kichocheo muhimu. Vilevile, utachangia moja kwa moja katika mafanikio ya Mpango Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na utekelezaji wa Sera ya Nishati ya mwaka 2015.
Kwa upande wake, Mhandisi John Bura, mmoja wa washiriki, aliupongeza mpango huo akisema utafungua fursa nyingi za uwekezaji. Hata hivyo, alitoa rai kwa serikali na taasisi za kifedha. "Ili mpango huu ufanikiwe, tunahitaji kuona mazingira wezeshi kwa wawekezaji, hasa wazawa. Kuharakisha upatikanaji wa mikopo kutawapa nguvu ya kujenga miundombinu itakayosambaza gesi hii kwa wananchi wengi zaidi na kwa haraka," alishauri Bura.