Mfumo wa Stakabadhi Ghalani Manyara Hatarini: RIVACU Yatoa Kilio Kizito kwa Rais Samia, Yataja 'Wateule' Kuhujumu Mfumo

economy | Sat Oct 25 2025


Mfumo wa Stakabadhi Ghalani Manyara Hatarini: RIVACU Yatoa Kilio Kizito kwa Rais Samia, Yataja 'Wateule' Kuhujumu Mfumo

Lile ambalo lilipaswa kuwa suluhu la kilio cha muda mrefu cha wakulima kuhusu bei, sasa linaonekana kugeuka kuwa chanzo kipya cha maumivu. Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, ambao ulianzishwa na Serikali ili kumkomboa mkulima kutoka kwenye mikono ya walanguzi, sasa unadaiwa kuwa katika hatari ya kuporomoka mkoani Manyara kutokana na hujuma zinazofanywa na kundi la wanunuzi binafsi.


Katika hali ya sintofahamu, wakulima na Chama chao Kikuu cha Ushirika (RIVACU) wamelazimika kutoa kilio chao hadharani, wakimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mara moja ili kunusuru jasho lao. Wakizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 25, viongozi wa wakulima hao wameeleza jinsi walanguzi wanavyonunua mazao yao kwa bei ya kutupa, na kuwaacha na hasara kubwa.


Mwenyekiti wa RIVACU, Bw. Yuda Sulle, alizungumza kwa uchungu akisema kumeibuka kundi kubwa la wanunuzi binafsi ambao wamepata usajili kwa wingi, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi. Alidai kuwa wanunuzi hao wanahujumu moja kwa moja mfumo rasmi wa stakabadhi ghalani ambao Serikali imekuwa ikiupigia chapuo kama njia bora ya kumpatia mkulima bei yenye tija.


Bw. Sulle alienda mbali zaidi na kuzituhumu mamlaka za usimamizi, akisema, "Hawa wanunuzi binafsi wanasajiliwa kiholera na kwa idadi kubwa. Wanapata baraka kutoka Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi Ghalani (WRRB) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko. Lengo lao ni moja tu: kuwahujumu wakulima."


Akipeleka ombi lake moja kwa moja Ikulu, Mwenyekiti huyo alimuomba Rais Samia kuingilia kati ili kudhibiti wimbi hili la wanunuzi binafsi, ambao alidai wanaingizwa kimkakati na baadhi ya 'wateule' ili kuvuruga soko na kuwanyonya wakulima. "Lengo lao kuu ni kumdidimiza mkulima. Tunamuomba Rais Samia afumbue macho na kulitazama jambo hili kwa uzito," alisisitiza Bw. Sulle.


Uchungu huu haukuishia kwa mwenyekiti pekee. Mwenyekiti wa Chama cha Kilimo na Masoko (AMCOS) cha Gendi, Bw. Gabriel Sillo, alieleza kuwa sera ya serikali ya stakabadhi ghalani iliyotumika msimu wa 2023/24 ilikuwa na mafanikio makubwa. Hata hivyo, msimu huu mambo yameharibika. "Tumekwazika sana baada ya kuona wanunuzi binafsi wanaruhusiwa kununua mazao yetu. Hili jambo linahujumu kabisa uchumi wa vyama vya ushirika na AMCOS zetu. Ombi letu ni kwamba hawa wanunuzi binafsi wapigwe marufuku kabisa," alisema Bw. Sillo.


Akiwasilisha ushahidi wa jinsi mfumo unavyohujumiwa, Meneja wa RIVACU, Bw. Pendael Valentine, alitoa takwimu za kulinganisha. Alieleza kuwa kwa zao la Ufuta, ambapo mfumo ulifanya kazi vizuri, walikuwa wamepanga kukusanya tani 1,500 kwa msimu wa 2025/26, lakini walivuka lengo na kufanikiwa kukusanya tani 2,600. Matokeo yake, wakulima walilipwa jumla ya Shilingi Bilioni sita.


"Lakini hali ni tofauti kabisa kwa zao la Dengu," alisema Bw. Pendael. "Mwaka huu tumekwama. AMCOS hazifanyi kazi kabisa kutokana na hawa wafanyabiashara binafsi kuingilia mfumo. Baadhi ya maghala yetu yamefungwa. Tunaomba Serikali iingilie kati kunusuru wakulima."


Mjumbe kutoka Karatu na Ngorongoro, Bw. Charles Golanga, aliongeza kuwa makubaliano ya awali yalikuwa kuwaruhusu wanunuzi binafsi kununua kiasi kidogo kwa ajili ya dharura, lakini sasa wamegeuka na kuanza kukusanya mazao yote kila kona.


Tuhuma nzito zaidi zilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Khabeera Co. Ltd, Bw. Mohamed Katindi, aliyehusisha hujuma hizo na mazingira ya kisiasa. "Wateule wa Rais ndio wanaharibu mfumo huu. Wanajua Rais yuko 'busy' na kampeni, hivyo wanatumia mwanya huo wakiamini hatawafanya kitu," alidai Katindi. Alipendekeza suluhu, akisema, "Ili kunusuru mfumo huu, ni vizuri Rais amtume Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo aje huku Manyara azungumze na RIVACU na wakulima."


Gazeti la Nipashe lilipomtafuta Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Sendiga, kuhusu madai haya, alisema alikuwa bado hajapata taarifa hizo rasmi. Hata hivyo, aliahidi kulifuatilia suala hilo kupitia wataalamu wake ili kubaini ukweli.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.