Maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii tiba Kusini mwa Jangwa la Sahara yameanza kuzaa matunda halisi, baada ya programu za majaribio za utalii tiba kufanikiwa kuingiza zaidi ya Shilingi bilioni mbili nchini.
Hayo yamebainishwa leo mjini Dodoma wakati Kamati ya Kitaifa ya Utalii Tiba ilipokabidhi ripoti yake ya miaka minne (2021-2024) kwa Waziri wa Afya, Jenista Mhagama. Akizungumza kwa niaba ya kamati, Makamu Mwenyekiti, Abdulmalik Mollel, alisema wazo la kuanzisha mkakati huu lilitokana na Rais Samia mwenyewe, baada ya kutembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Mei 2021 na kuridhishwa na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika vifaa vya kisasa.
"Rais Samia alisema anatamani kuona Tanzania inakuwa kituo cha tiba utalii. Kamati yetu ilizaliwa kutokana na maono hayo," alisema Mollel.
Kamati hiyo ilipewa jukumu la kuangalia uwezo wa Tanzania na kupendekeza njia za kutekeleza maono hayo. Walifanya ziara za kimafunzo katika nchi zilizoendelea kwenye utalii tiba kama India, na kuteua hospitali nne za majaribio: Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), JKCI, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), na Taasisi ya Mifupa (MOI).
Akithibitisha mafanikio hayo kwa vitendo, Mkurugenzi wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, alitoa mfano wa programu maalum ya "Dk. Samia Outreach" iliyofanyika nchini Comoro. Alisema kwa kutumia gharama ya Shilingi milioni 300 kutangaza huduma za Tanzania, wamefanikiwa kuwavutia wagonjwa ambao hadi sasa wamelipia matibabu yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni mbili.
"Maana yake hizi fedha zilizopatikana zinarejea kwenye mfumo na kusaidia kugharamia matibabu kwa Watanzania wasio na uwezo. Huu ni ushahidi kuwa uwekezaji huu una manufaa makubwa," alisema Dk. Kisenge.
Akipokea ripoti hiyo, Waziri Mhagama aliipongeza kamati na kusisitiza kuwa ili kufanikiwa kikamilifu, sekta ya afya inapaswa kuwekeza kwenye ukarimu na huduma bora kwa wateja, kama mashirika ya ndege ya kimataifa. "Mgonjwa anapofika na kupokelewa kwa tabasamu, tayari anaanza kupata nafuu. Ukarimu ni sehemu ya tiba," alisema Mhagama.
Waziri Mhagama alimalizia kwa kuahidi kuunda kamati mpya itakayoendeleza kazi hiyo, huku akimpongeza na kumwomba Bw. Mollel kuendelea kuwa sehemu ya uongozi wa jitihada hizo kutokana na mchango wake mkubwa.