Hekaheka za kibiashara zimetawala katika Uwanja wa Jamhuri uliopo katikati ya mji wa Morogoro, huku serikali ikiwakumbusha wafanyabiashara na wananchi kuwa mtaji namba moja wa maendeleo ya kiuchumi si fedha, bali ni amani na utulivu wa nchi.
Hayo yamebainishwa jana wakati wa ufunguzi rasmi wa Maonesho ya Biashara Mkoa wa Morogoro (Morogoro Region Trade Fair - MRTFE), tukio ambalo limekutanisha wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa chini ya uratibu wa Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) kwa kushirikiana na serikali. Maonesho hayo yaliyoanza Novemba 20, yanatarajiwa kuhitimishwa kishindo Novemba 30 mwaka huu.
"Pesa Inaogopa Kelele" Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Musa Kilakala, amesisitiza kuwa mazingira wezeshi ya biashara yanategemea sana usalama wa taifa. Kilakala amewataka wakazi wa Morogoro na Watanzania kwa ujumla kuilinda amani kama mboni ya jicho, akionya kuwa vurugu zikitokea, sekta ya biashara ndiyo huwa ya kwanza kuumia.
"Ndugu zangu, amani ndiyo msingi wa kila kitu. Bila amani, hata haya maonesho mazuri tunayoyaona leo yasingewezekana. Mjasiriamali hawezi kuleta bidhaa zake uwanjani kama hakuna usalama. Hivyo, ni wajibu wetu sote kuimarisha tunu hii ili uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa uzidi kupaa," alisisitiza Kilakala huku akipigiwa makofi na wafanyabiashara waliofurika uwanjani hapo.
TCCIA na Soko la Bilioni 1.4 Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu wa TCCIA, Oscar Kisanga, ametumia jukwaa hilo kuwapa "shule" wafanyabiashara kuhusu fursa zinazowasubiri nje ya mipaka. Kisanga amewahamasisha wajasiriamali kujiunga na chemba hiyo ili waweze kuunganishwa na masoko ya kimataifa na fursa za mikopo yenye masharti nafuu.
Kisanga amefichua kuwa TCCIA ipo katika hatua nzuri za kimkakati kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na Soko Huru la Afrika (AfCFTA). "Tunayatazama maono ya mwaka 2030 ambapo soko la Afrika litakuwa na walaji zaidi ya bilioni 1.4. Hii ni fursa ya kipekee. Nawaomba mzalishe bidhaa zenye ubora ili muweze kushindana na kuuza katika soko hili kubwa badala ya kuishia kuuziana wenyewe kwa wenyewe hapa ndani," alieleza Kisanga.
Morogoro Yapaa Kimapato Habari njema zaidi katika maonesho hayo zilitoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Ofisa Mwandamizi wa Elimu na Mawasiliano wa TRA Mkoa wa Morogoro, Immaculate Chaggu, amemwaga sifa kwa wafanyabiashara wa mkoa huo kwa uzalendo wao wa kulipa kodi bila shuruti.
Bi. Chaggu amebainisha kuwa mwamko huo umewezesha mkoa wa Morogoro kuvuka lengo la makusanyo kwa mwaka 2025 kwa zaidi ya asilimia 100. "Tunajivunia sana wafanyabiashara wa Morogoro. Elimu tunayotoa kila Alhamisi imezaa matunda. Watu wanalipa kodi kwa hiyari na matokeo yake mkoa wetu unavuka malengo na kuchangia kikamilifu kwenye kapu la taifa," alisema.
NSSF: Wajasiriamali Msisahau Uzeeni Wakati biashara zikiendelea, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) nao haukuwa nyuma. Ofisa Matekelezo wa NSSF Mkoa wa Morogoro, Mema Kabaiza, aliwakumbusha wajasiriamali kuwa biashara inaweza kupanda na kushuka, hivyo ni muhimu kujiwekea akiba.
Kabaiza aliwasihi kujiunga na mfuko huo ili wapate uhakika wa matibabu kupitia bima ya afya na pensheni ya uzeeni, akisisitiza kuwa gharama za matibabu zimepanda na bima ndiyo mkombozi pekee kwa mjasiriamali na familia yake.
Maonesho haya ya Morogoro yanaendelea kuwa kioo cha uchumi wa mkoa huo, yakionesha namna ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, na taasisi za kifedha unavyoweza kuleta tija kwa mwananchi wa kawaida.