Katika hatua inayolenga kuondoa vikwazo na kero sugu zinazowakabili wafanyabiashara mkoani Manyara, Mkuu wa Mkoa huo, Queen Sendiga, ametoa maagizo mazito kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha dawati maalum la uwezeshaji biashara lililozinduliwa linafanya kazi kwa tija na uwazi.
Sendiga ameweka msisitizo kuwa hataki kuona dawati hilo linakuwa la maonyesho, bali chombo halisi cha kutatua changamoto na kulea biashara mpya. Ili kuhakikisha hilo, ameagiza kuletewa taarifa ya kina ya utendaji wa dawati hilo kila mwezi. Taarifa hiyo itapaswa kuonyesha idadi kamili ya wafanyabiashara waliohudumiwa, changamoto zao, na jinsi zilivyotatuliwa.
"Kila mwezi nataka ripoti iwe mezani kwangu. Inioneshe ni wafanyabiashara wangapi wamekuja, kero gani zinalalamikiwa zaidi, na mmeweka mkakati gani kuhakikisha hazijirudii. Vilevile, nataka kuona matokeo chanya, biashara ngapi mpya zimeanzishwa kupitia ushauri wenu na mchango wake katika kupanua wigo wa walipa kodi," alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa wakati wa uzinduzi rasmi leo, Septemba 12.
Aidha, alitoa onyo kwa watumishi wa TRA kuepuka dharau na kubeza malalamiko ya wafanyabiashara, akisema hata kero inayoonekana ndogo inaweza kuwa kikwazo kikubwa kwa mjasiriamali.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Manyara, Alex Katundu, alikiri kuwepo kwa changamoto kama urasimu katika usajili wa biashara na uelewa mdogo miongoni mwa wajasiriamali. Alisema dawati hilo jipya litafanya kazi kwa karibu na wafanyabiashara, kutoa elimu, na kuwasogezea huduma ili kurahisisha shughuli zao.
Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) mkoani humo, kupitia kwa Mwenyekiti wake Musa Msuya, kimeipongeza serikali kwa hatua hii, kikisema ni ishara ya dhamira ya kweli ya kuboresha mazingira ya biashara na kujenga daraja la lugha moja kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.