Historia mpya imeandikwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati baada ya serikali za Tanzania na Burundi kuzindua rasmi ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) itakayounganisha nchi hizo mbili. Katika hafla iliyofanyika Jumamosi, Agosti 16, 2025, nchini Burundi, Rais wa nchi hiyo, Évariste Ndayishimiye, aliungana na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya kipande cha Uvinza (Tanzania) hadi Msongati (Burundi), mradi wenye thamani ya zaidi ya dola za Kimarekani bilioni mbili.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa, aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, alisema mradi huo ni alama thabiti ya ukuaji wa uchumi na ushirikiano wa kikanda, unaotimiza ndoto ya muda mrefu ya kuziunganisha nchi za Afrika. Alisema reli hiyo itaongeza kasi ya ukuaji wa sekta za kilimo na madini, na itaimarisha uhusiano wa kindugu kati ya Tanzania na Burundi ulioanza tangu mwaka 1975.
Ujenzi wa reli hii unatazamiwa kuleta mapinduzi katika sekta ya usafirishaji. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alifafanua kuwa gharama za kusafirisha kontena la tani 20 kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi Burundi zitashuka kwa karibu nusu, kutoka dola 3,800 za sasa hadi dola 2,000. Zaidi ya hayo, treni moja ya SGR itakuwa na uwezo wa kubeba tani 3,800 za mizigo kwa wakati mmoja, sawa na uwezo wa zaidi ya malori 120.
"Mradi huu utapunguza kwa kiasi kikubwa athari za hewa ya ukaa kwa sababu treni itatumia umeme, na unatekeleza ajenda ya Afrika ya kuwa na mtandao wa reli za kisasa ifikapo mwaka 2063," alisema Prof. Mbarawa. Aliongeza kuwa mradi huo, unaotekelezwa na mkandarasi CR Consortium, unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka sita, huku akitoa shukrani kwa Benki ya CRDB kwa kutoa dola milioni 100 kama fedha za kuanzia.
Mradi huu unapata ufadhili mkubwa kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ambayo imeusifu kama mradi wa kimkakati utakaotatua changamoto nyingi za kibiashara. Kwa upande wake, Rais Ndayishimiye wa Burundi aliishukuru Tanzania kwa ushirikiano wake wa kidugu, akitolea mfano kitendo cha Tanzania kuipa Burundi eneo maalum katika bandari kavu ya Katosho, Kigoma, kwa ajili ya mizigo yao.