Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeitaka Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi kuharakisha kukamilisha mchakato wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika Kijiji cha Msungua, kilichopo wilayani Singida. Aidha, tume hiyo imeagizwa kutoa hati miliki za kimila kwa wakazi wa kijiji hicho mara baada ya kukamilika kwa mpango huo.
Agizo hilo lilitolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Timotheo Mzava, baada ya kamati yake kutembelea kijiji hicho na kukagua maendeleo ya zoezi la upangaji wa matumizi bora ya ardhi kwa wakazi. Mheshimiwa Mzava alisema kuwa kamati yake imeridhishwa na kasi ya kazi inayofanyika hadi sasa. Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa hatua zote zinazohitajika katika mchakato huo zinakamilishwa ili wananchi waanze kunufaika na mpango huo haraka iwezekanavyo.
"Sisi kama kamati tumeridhika na kasi ya kazi hii. Ushauri wetu kwa sasa, tunapoelekea katika maeneo mengine ambako mtafanya mipango bora ya matumizi ya ardhi, ni kuhakikisha mnakamilisha hatua zote zinazotakiwa ili wananchi waanze kunufaika," alisisitiza Mheshimiwa Mzava.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Geofrey Pinda, aliwahimiza wananchi wa Msungua ambao wamenufaika na mpango huo kulinda maeneo yao ya ardhi kwa ajili ya kuinua uchumi wao. Alieleza kuwa mara nyingi maeneo mengi yanakosa huduma muhimu za kijamii kutokana na ukosefu wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Alitoa mfano wa baadhi ya vijiji ambavyo vinakataa kabisa kutenga ardhi kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, na badala yake wanawaambia viongozi wa serikali kuwa wanapaswa kununua ardhi.
"Tunawawekea mpango huu ili uwasaidie. Kwa hiyo, jitahidini kuyatunza maeneo yenu," alisisitiza Naibu Waziri Pinda. Aliongeza kuwa mpango wa matumizi bora ya ardhi una manufaa mengine mengi, ikiwa ni pamoja na kusaidia kupunguza migogoro ya ardhi miongoni mwa wananchi.
Wakazi wa Kijiji cha Msungua walionyesha shukrani zao kwa serikali kwa kuwapelekea mpango huo. Walisema kuwa mpango huo umewasaidia sana kupunguza migogoro ya ardhi iliyokuwa ikiwakabili hapo awali. Bi Halima Athumani, akizungumza kwa niaba ya wakazi wenzake, alisema kuwa mpango wa matumizi bora ya ardhi ni mzuri sana kwani unaelekeza wazi matumizi mbalimbali ya ardhi. "Mpango huu unaelekeza wakulima tutalima wapi, wafugaji watafuga wapi, wapi ni makazi, wapi kutakuwa na huduma za jamii kama shule na zahanati, na wapi kutakuwa na barabara," alieleza Bi Athumani.