Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imeleta habari njema kwa walimu wa shule za sekondari wilayani humo baada ya kuanzisha utaratibu wa kutoa motisha ya fedha taslimu kwa kutambua juhudi zao katika kuinua kiwango cha taaluma. Kuanzia sasa, mwalimu yeyote ambaye mwanafunzi wake au wanafunzi wake watapata alama ya 'A' katika somo analofundisha kwenye mitihani ya kitaifa ya sekondari, atazawadiwa kiasi cha Shilingi 10,000 kwa kila alama 'A' hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla maalum ya pongezi kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa, Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Sekondari katika Halmashauri hiyo, Bi. Hellen Mselem, alisema uamuzi huo umefikiwa kwa kuzingatia kuwa zawadi ya fedha ni njia nzuri ya kuthamini mchango wa mwalimu na ni kichocheo kinachoweza kumfanya ajisikie ametambuliwa na kuthaminiwa katika wilaya hiyo.
Bi. Mselem alifafanua kuwa lengo la kutoa motisha hizo ni kutambua na kuthamini juhudi za walimu katika kuwezesha wanafunzi kufanya vizuri kwenye mitihani ya kumaliza kidato cha sita, kidato cha nne, pamoja na mitihani ya upimaji wa utendaji kwa kidato cha pili. "Tunaangalia na kuthamini ni jinsi gani mwalimu amejitahidi sana kuwezesha matokeo kuwa mazuri. Anajisikia faraja amethaminiwa katika kazi yake," alisema Bi. Mselem.
Aliongeza kuwa wanaamini motisha hii mpya itajenga hamasa kubwa kwa walimu na kuwahamasisha kuendelea kujituma zaidi katika kazi zao na hatimaye kuleta matokeo bora zaidi kielimu.
Akielezea jinsi mpango huo utakavyotekelezwa, Bi. Mselem alibainisha kuwa walimu waliopata alama 'A' katika masomo yao watalipwa Shilingi 10,000 kwa kila 'A' moja. Alitoa mfano, akisema "Kwa hiyo, walimu waliopata A katika masomo yao kwa kila somo moja, sisi Halmashauri kupitia OC (fedha za matumizi mengineyo), Mkurugenzi Mtendaji, ametoa fedha na ameelekeza wapewe Shilingi 10,000 kwa kila A moja. Hivyo kama amepata A 10 maana yake anapata Shilingi 100,000."
Mpango huu wa motisha kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Hai unatarajiwa kuwa mfano kwa halmashauri nyingine nchini katika kutambua na kuwekeza katika juhudi za walimu, ambao ni nguzo muhimu katika kuinua kiwango cha elimu na kuandaa vizazi vijavyo vya taifa. Ni hatua inayoonyesha jinsi viongozi wa serikali za mitaa wanavyoweza kutumia rasilimali zilizopo kuhamasisha utendaji bora katika sekta muhimu kama elimu.