Serikali nchini Tanzania imewaonya vikali watoa huduma za afya, hususan wauguzi na wakunga, dhidi ya tabia ya kuomba au kupokea hongo kabla au baada ya kutoa huduma kwa wananchi. Onyo hili limetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Saitore Laizer, alipokuwa akizungumza na wauguzi na wakunga wapatao 257 waliohitimu mafunzo yao kupitia ufadhili wa Shirika la Camfed Tanzania. Wahitimu hawa walikuwa wakisoma katika vyuo 20 vya afya vilivyoko sehemu mbalimbali za nchi.
Dkt. Saitore alisisitiza kuwa endapo mtumishi yeyote katika kada hii atafanya uzembe au ukiukaji wa maadili katika utoaji wa huduma, lawama hazitamuelemea yeye pekee bali zitaikumba tasnia nzima ya afya. Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuwekeza kwa nguvu katika sekta ya afya kwa kuhakikisha kuwa watumishi wanapata mazingira bora ya kazi. Sambamba na hilo, serikali imeahidi kuendelea kuboresha miundombinu ya hospitali, vituo vya afya, na zahanati ili kuwawezesha watoa huduma kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Alieleza kuwa elimu waliyoipata ni chachu ya mabadiliko makubwa katika maisha yao binafsi na kwa jamii kwa ujumla, akiongeza kuwa kazi ya uuguzi na ukunga ni uti wa mgongo wa sekta ya afya nchini.
Kwa upande wake, Mratibu wa Ufadhili wa Uuguzi na Ukunga, ambaye pia ni afisa wa Camfed Mkoa wa Tanga, Bi. Tukaeje Mzeru, alieleza kuwa mwaka 2021, shirika hilo lilipata ufadhili kwa ajili ya kusaidia wasichana wanaotoka katika mazingira magumu wanaosoma katika eneo hilo. Mpango huo ulikuwa wa miaka minne na ulihusisha nchi za Tanzania na Ghana.
Bi. Mzeru alifafanua kuwa lengo kuu la ufadhili huo ni kuongeza idadi ya wataalamu wa afya, hasa katika maeneo ya vijijini. Hii inalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote na kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa ujauzito na kujifungua. Alisema, "Camfed kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, walikubaliana kutumia vyuo 20 vya afya kwa ajili ya mafunzo haya. Mpango huu ulilenga kuwafikia wasichana 280 nchini Tanzania kwa kuwagharamia ada za masomo, malazi, chakula, vifaa vya kujifunzia, na usafiri, ili kuhakikisha wanaendelea na masomo yao bila vikwazo vya kifedha."
Mratibu huyo aliongeza kuwa takriban shilingi bilioni 4.2 za Tanzania zimetumika kuwafadhili wanafunzi 298, ambapo 257 kati yao ndio waliohitimu hivi karibuni.
Mkurugenzi wa Camfed, Bw. Nasikiwa Duke, alisema kuwa shirika hilo lina lengo la kufikia na kufadhili mabinti 2,000. Alisisitiza kuwa msukumo wa kufadhili wasichana hawa unatokana na mpango wao wa kuongeza idadi ya wahudumu wa afya ili kuhakikisha jamii za pembezoni zinapata huduma za afya kwa haraka na kwa ufanisi.
Naye mmoja wa wauguzi waliohitimu, Bi. Janeth Charles, alisema kuwa wao wamejiandaa kikamilifu kwenda kuhudumia jamii kwa kuzingatia elimu waliyoipata, hasa kwa kuwafikia watu wanaoishi katika maeneo ya mbali ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi za kupata huduma za afya.