Ukatili wa kijinsia unaendelea kusababisha maafa nchini, huku chanzo kikuu cha kuendelea kwa matukio hayo kikitajwa kuwa ni usiri unaotumiwa kama kichaka. Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dkt. Roses Reuben, wakati wa majadiliano kuhusu hali ya ukatili wa kijinsia nchini yaliyofanyika Dar es Salaam chini ya Mradi wa Sauti zetu.
Dkt. Rose alieleza kuwa hofu ya kutoa taarifa za ukatili inatokana na kuwepo kwa siri za familia, jambo ambalo linapelekea watoto kubakwa, kunajisiwa, au kulawitiwa kisha kutishiwa na kukubali ibaki kuwa siri. Usiri huu umesababisha watu kadhaa kupoteza maisha au kupata ulemavu wa kudumu.
Majadiliano hayo yalikusanya wadau mbalimbali, ikiwemo wanafunzi, walimu, wanawake wajasiriamali, wanaharakati, na waandishi wa habari.
Madhara ya Kisayklojia na Afya ya Akili
Mwezeshaji Frank Sanga alibainisha kuwa mbali na wahanga, hata waandishi wa habari wanaweza kupata madhara ya kisaikolojia wanaporipoti matukio ya ukatili. Pia, alionya kuwa aina fulani ya uandishi wa habari inaweza kuchochea kuongezeka kwa matukio hayo, na hivyo vyombo vya habari vinapaswa kutafakari upya mbinu zao.
Sanga alitaja mambo kadhaa yanayochochea vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na mauaji:
- Afya ya akili
- Migogoro ya kifamilia na wazazi kutendeana vibaya
- Ugumu wa maisha
- Kifo cha mzazi/wazazi
- Kusahau Mungu
Umhimi wa Kuripoti Haraka na Matibabu ya Dharura
Halili Katani, Afisa Ustawi Mwandamizi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, alisisitiza umuhimu wa watu wanaofanyiwa ukatili kuripoti matukio haraka kwenye vituo husika.
Alifafanua kuwa kwa waliobakwa, kuna huduma muhimu za dharura zinazotolewa, ikiwemo dawa za kuzuia mimba na dawa za kudhibiti maambukizi ya virusi vya UKIMWI (ARVs), na pia huanzishiwa matibabu mapema.
Katani alieleza kuwa maafisa ustawi wanawapokea na kuwapa msaada wa haraka manusura. Hata kama manusura anawahi hospitali bila fomu namba 3 inayotolewa na polisi, husaidiwa kupata matibabu kwanza kisha utaratibu wa fomu hiyo hufanywa. Alisisitiza kuwa kumwokoa manusura ni muhimu zaidi kuliko kufuata hatua za kisheria pekee.
"Ikiwa manusura ni mtoto mdogo, hawezi kuhojiwa akiwa pekee yake, lazima Afisa Ustawi wa Jamii awepo," alisisitiza Katani, akisisitiza umuhimu wa kulinda usalama wa manusura.
Janeth Mawinza, Mkurugenzi wa asasi ya Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), alihimiza juhudi za kuelimisha jamii, hasa wanaume, kuwa walinzi wa watoto na kufuatilia mazingira yao ili kuwasaidia watoto kuongozwa mahali salama.