Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetoa wito kwa jamii nzima ya Watanzania kushiriki kikamilifu katika juhudi za upandaji miti na usimamizi endelevu wa misitu. Hatua hii inatambuliwa kama nguzo muhimu ya kulinda vyanzo vya maji, kuhifadhi bioanuwai, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, na kukuza uchumi wa taifa.
Akizungumza leo, muda mfupi kabla ya ufunguzi wa Siku ya Mazingira kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Meneja wa Sehemu ya Baiolojia ya Mbegu za Miti TFS, Bw. Fandey Mashimba, amesema Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha upandaji miti unakuwa endelevu na wenye tija.
Kwa mujibu wa Mashimba, Tanzania Bara inakadiriwa kuwa na hekta milioni 48.1 za misitu, ambayo ni sawa na asilimia 55 ya eneo lote la ardhi. Kati ya misitu hiyo, zaidi ya nusu inasimamiwa na serikali kuu, serikali za vijiji, na mamlaka za mitaa, jambo linaloashiria umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi.
Hata hivyo, Mashimba alionya kuhusu upotevu mkubwa wa misitu nchini. "Kwa mwaka, tunakadiria upotevu wa hekta zaidi ya 469,000 kutokana na kilimo cha kuhamahama, uvunaji haramu wa mazao ya misitu, na matumizi yasiyodhibitiwa ya kuni na mkaa. Upandaji miti wa kimkakati ndio suluhisho pekee, hivyo ni lazima tupande miti kwa wingi na miti sahihi kulingana na ikolojia za maeneo husika," alisisitiza Mashimba.
Aliwataka wananchi, sekta binafsi, na washirika wa kimataifa kushirikiana na TFS na serikali kwa ujumla katika juhudi za uwekezaji katika miradi ya upandaji miti. Pia, aliwahimiza kutunza miti hiyo ili iweze kusaidia misitu iliyopo katika kulinda vyanzo vya maji, kukabiliana na upungufu wa rasilimali za misitu, na kuboresha mifumo ya ikolojia. Mashimba alisisitiza umuhimu wa kutumia mbegu bora za miti zinazotoka kwenye misitu ya kupanda na ile asili.
Zaidi ya hayo, Mashimba alifafanua kuwa TFS inahitaji miche milioni 440 kila mwaka ili kufikia lengo la kurejesha ardhi iliyoharibiwa na kutimiza ahadi za kitaifa na kimataifa, kama vile AFR100, ambapo TFS ni mratibu wa Kitaifa. Alisema wazi kuwa bila ushiriki wa wadau wengine, kufanikisha lengo hili muhimu itakuwa changamoto kubwa.
Mbali na kuhifadhi maji na bioanuwai, Mashimba alisisitiza kuwa misitu inatoa ajira na kipato kupitia biashara ya mazao ya misitu, ufugaji nyuki, na utalii wa ikolojia. Alitaja pia miradi ya kaboni kama fursa muhimu ya mapato na kupunguza gesi joto, huku akisisitiza haja ya kutoa elimu kwa jamii ili mikataba inayoingiwa ifuate miongozo ya kitaifa na kimataifa kwa maslahi ya nchi na jamii zinazozunguka misitu hiyo.
Katika kampeni za upandaji miti, Mashimba alitaja changamoto mbalimbali zinazojitokeza, ikiwemo vifo vya miche kutokana na uangalizi hafifu, hasa katika maeneo ya vijijini. Nyingine ni ushiriki mdogo wa sekta binafsi, kutokuwepo kwa mipango ya matumizi bora ya ardhi, pamoja na migogoro ya ardhi. Ili kukabiliana na changamoto hizi, TFS inaendelea kushirikisha serikali, asasi za kiraia, na taasisi za utafiti kama vile Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) ili kuimarisha juhudi za pamoja.
Mashimba alimalizia kwa kusisitiza kuwa ushirikiano wa wadau wote ni muhimu ili Tanzania ibaki kuwa ya kijani kwa vizazi vijavyo. "Misitu ni uhai wa sekta nyingine kama vyanzo vya maji na uchumi wa misitu. Upandaji na utunzaji wa miti ni msingi wa uhifadhi wa mazingira na unachangia kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa," alihitimisha.