TAMISEMI Yawapa Wahitimu wa Kidato cha Nne Mwezi Mmoja Kubadili Tahasusi

culture | Thu Apr 03 2025


TAMISEMI Yawapa Wahitimu wa Kidato cha Nne Mwezi Mmoja Kubadili Tahasusi

Serikali ya Tanzania, kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imetoa muda wa mwezi mmoja kwa wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2024 kubadili tahasusi au kozi walizochagua awali.


Muda huo wa mwezi mmoja ulianza Machi 31 na utaisha Aprili 30, mwaka huu. Hii ni fursa muhimu kwa wanafunzi kufanya marekebisho katika machaguo yao ya elimu ya juu.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, alisema kuwa serikali imetoa fursa kwa wanafunzi kubadili machaguo yao ya tahasusi za kidato cha tano na kozi za vyuo vya kati na elimu ya ufundi kupitia mfumo wa kielektroniki wa uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha tano na vyuo.


"Hatua hii ni maandalizi ya awali ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga Kidato cha Tano na Vyuo vya Serikali kwa mwaka 2025," alisema Mchengerwa alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana.


Alisema kuwa serikali, kupitia Ofisi ya Rais - TAMISEMI, imekamilisha mchakato wa awali wa kuingiza kwenye kanzidata taarifa zote zilizomo kwenye fomu za uchaguzi za wanafunzi, kama zilivyoandikwa na wanafunzi wenyewe wakiwa shuleni.


"Baada ya wanafunzi kufanya marekebisho yao, kanzidata hiyo ndiyo itakayotumika kuwachagua na kuwapangia nafasi za Kidato cha Tano na Kozi mbalimbali katika Vyuo vya Kati na vya Elimu ya Ufundi, kwa kuzingatia sifa za ufaulu na machaguo yao," alisisitiza Mchengerwa.


Aliongeza: "Ofisi ya Rais - TAMISEMI inatoa fursa kwa wahitimu wa elimu ya sekondari Kidato cha Nne, mwaka 2024, kubadili machaguo yao ili kutoa nafasi zaidi kwa mwanafunzi kusoma tahasusi au kozi itakayomwandaa kuwa na utaalamu stahiki katika maisha yake ya baadaye."


Mchengerwa alisema kuwa hatua hii pia itawapa wanafunzi fursa zaidi ya kuongeza machaguo yao na kufanya machaguo mapya ya tahasusi na kozi wanazopenda.


"Napenda kuwasihi wazazi na walezi kushauriana kwa kina na watoto wao na kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kufanya machaguo sahihi ya tahasusi na kozi kulingana na ufaulu wao," alisema.


Aliwahimiza wanafunzi, wazazi na walezi kushauriana kwa kina, ikiwa ni pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu na kitaaluma, kabla ya kufanya mabadiliko yoyote ya tahasusi au kozi.


Mchengerwa aliwataka wahitimu kufanya marekebisho ya machaguo yao ya tahasusi na kozi kulingana na ufaulu wao kwa kuingia kwenye mfumo wa uchaguzi wa wanafunzi, ambao unapatikana kupitia kiunganishi cha tovuti cha selform.tamisemi.go.tz.


Alisema kuwa mhitimu anapaswa kuandika jina lake la mwisho, mwaka wa kuzaliwa, na alama za ufaulu alizopata kwenye somo atakaloulizwa na mfumo, au swali lolote litakaloulizwa.


"Ni matumaini yangu kuwa wahitimu wote watatumia kwa ukamilifu fursa waliyopewa ya kubadilisha tahasusi na kozi kulingana na ufaulu waliopata. Pia, wataweza kusoma tahasusi au kozi ambazo wamefaulu vizuri au wana malengo nazo zaidi," alisema Mchengerwa.


Alisema kuwa baada ya kukamilika kwa utaratibu huo na wanafunzi kupangiwa shule na vyuo, hakutakuwa na fursa tena kwa wazazi na wanafunzi kubadili tahasusi na kozi zao.


"Ninawasisitiza wanafunzi, wazazi na walezi kutumia muda huo vyema ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza mara baada ya matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo kutangazwa," alisema Mchengerwa.


Aliongeza: "Baada ya matokeo ya kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo kutangazwa, huduma ya kubadilisha tahasusi na kozi itakuwa bure."

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.