Kwa miaka mingi, wakazi wa vijiji vinavyopakana na maeneo ya hifadhi katika Wilaya ya Itilima, Mkoa wa Simiyu, wameishi na kero ya migogoro na wanyamapori wakali. Changamoto haikuwa tu kupoteza mazao na maisha, bali pia urasimu na ucheleweshaji wa malipo ya kifuta jasho/machozi kutoka serikalini. Hata hivyo, sasa neema imewashukia kufuatia kuanzishwa kwa mfumo mpya wa kidijitali wa kuripoti matukio hayo.
Serikali, kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, imebuni na kuboresha Mfumo wa Ukusanyaji Taarifa za Wanyamapori Waharibifu (PAIS), ambao umepokelewa kwa shangwe na wananchi wa vijiji vya Nyantugutu, Lung'wa na Nding'ho. Mfumo huu umekata minyororo ya urasimu na kurahisisha mchakato mzima wa malipo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara kijijini Nding'ho mnamo Oktoba 9, 2025, Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Bi. Salome Kambona, aliipongeza serikali kwa hatua hiyo. "Tunaishukuru sana Serikali. Mfumo huu mpya unamtaka mwananchi atoe taarifa ndani ya siku saba tu baada ya kupata madhara, na mchakato wa malipo unaanza mara moja. Hii ni hatua kubwa," alisema Kambona.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Bwana Mosses Saguda, mkazi wa Kijiji cha Nyantugutu, ambaye alishuhudia jinsi mfumo wa zamani ulivyokuwa wa kero. "Zamani tulikuwa tunakaa hata mwaka mzima bila kulipwa na ilikuwa ni usumbufu kufuatilia. Sasa hivi, kupitia PAIS, malipo yanafanyika haraka na fedha inaingia moja kwa moja kwenye simu au benki," alieleza Saguda. Pamoja na shukrani, aliomba serikali pia iangalie uwezekano wa kulipa kifuta jasho kwa mazao yanayoharibiwa na wanyama yakiwa yamehifadhiwa ghalani.
Mbali na mfumo huo, serikali inatoa elimu kwa jamii hizi kuhusu namna bora ya kuishi na wanyamapori na kuepuka migogoro. Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka wizarani, Nassoro Wawa, alisema serikali inatarajia wananchi sasa watajua taratibu za kufuata wanapopata madhara.
Zaidi ya hayo, aliwahimiza wananchi kugeuza uwepo wa wanyamapori kuwa fursa ya kiuchumi. "Sheria zetu zinaruhusu wananchi kuwekeza katika sekta hii. Mnaweza kuanzisha bucha za nyamapori, mashamba ya kufuga wanyama, au bustani za wanyama. Hii itawapa kipato na kupunguza utegemezi," alisisitiza Wawa. Elimu hii imekuja wakati muafaka kutokana na kuongezeka kwa matukio ya tembo, fisi, mamba na viboko katika maeneo hayo.