Serikali imechukua hatua madhubuti ya kupunguza athari za utengano wa familia kwa watumishi wa umma kwa kupanga kutoa vibali zaidi ya 200 vya uhamisho wiki ijayo. Hatua hii inalenga kuwasogeza watumishi hao karibu na familia zao, ambazo zimekuwa zikiathirika kutokana na wanandoa kuishi katika maeneo tofauti kwa muda mrefu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bwana George Simbachawene, alieleza hayo leo wakati wa kikao kazi na Wakuu wa Taasisi za Umma. Alibainisha kuwa baadhi ya watumishi wameishi mbali na familia zao kwa zaidi ya miaka 20, hali inayosababisha matatizo makubwa katika ndoa zao na malezi ya watoto.
Bwana Simbachawene aliwataka wakurugenzi wa halmashauri kuonyesha huruma na kutumia busara katika kushughulikia maombi ya uhamisho, hasa kwa watumishi wanaokaribia kustaafu. Alisema: “Wapo watumishi ambao tangu waanze kazi, ndoa zao zina miaka 20 lakini hawajawahi kuishi na wenza wao kwa zaidi ya mwezi mmoja. Mkurugenzi wa Halmashauri anamzuia mtu kutekeleza ombi lake la uhamisho hata kama amekaa sehemu moja kwa muda mrefu. Hata anapokaribia kustaafu, busara inahitajika ili apate nafasi ya kujenga familia yake.”
Aliongeza kuwa utengano wa wanandoa husababisha changamoto katika malezi ya watoto na ustawi wa familia kwa ujumla. Alitoa mfano wa watumishi wanaokaribia kustaafu na wanaotaka kurudi nyumbani kwa ajili ya kuandaa maisha yao ya baadaye, akisisitiza kuwa maombi yao yanapaswa kushughulikiwa kwa huruma na uelewa.
Waziri huyo alieleza kuwa serikali inajipanga kuhakikisha mchakato wa uhamisho unatekelezwa kwa ufanisi. Alisisitiza kuwa ajira mpya zitakazotolewa kupitia TAMISEMI zitasaidia kuziba nafasi za waliopata uhamisho.
“Tunatarajia kutoa vibali kwa zaidi ya watumishi 200 ambao mchakato wao wa uhamisho umekamilika. Nawaomba muwasiliane na TAMISEMI mnapopokea ajira mpya, kwani zitasaidia kuziba mapengo ya uhamisho wa watumishi waliopata nafasi ya kusogea karibu na familia zao. Kuna takribani watumishi 20,000 waliokaa katika vituo vyao vya kazi kwa muda mrefu, nawaomba muwe na busara katika kushughulikia maombi yao ili kuokoa ustawi wa familia hizi,” alisisitiza Bwana Simbachawene.
Hatua hii ya serikali inalenga kuimarisha maisha ya watumishi wa umma na kuongeza ari ya kufanya kazi kwa ufanisi, huku ikizingatia umuhimu wa mshikamano wa kifamilia.