Rais Samia Atoa Zawadi za Eid na Pasaka kwa Vituo vya Ustawi wa Jamii

culture | Sat Mar 29 2025


Rais Samia Atoa Zawadi za Eid na Pasaka kwa Vituo vya Ustawi wa Jamii

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa zawadi ya sukari kilo 2,500 na katoni 83 za maji kwa ajili ya sikukuu ya Eid Al-Fitr na Pasaka kwa vituo 24 vinavyotoa huduma za ustawi wa jamii, ikiwa ni pamoja na makao ya watoto ya Kurasini.


Vituo vingine vilivyopokea zawadi hizo ni mahabusu za watoto, makazi ya wazee, na Chuo cha Watu Wenye Ulemavu cha Yombo.


Akizungumza jijini Dar es Salaam Machi 28, 2025, kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa hafla ya utoaji wa zawadi hizo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, alisema Rais Samia ameendelea kuonyesha kujali makundi maalum kwa kutoa msaada wa zawadi mbalimbali kwa watoto, wazee, na watu wenye ulemavu katika vituo vyote vya ustawi wa jamii.


Alisema kati ya zawadi hizo, sukari kilo 500 zitaelekezwa Zanzibar, huku kilo 2,000 zikibaki Tanzania Bara, pamoja na maji.


"Katika mwaka wa fedha 2024/25, jumla ya shilingi milioni 165,317,000 zimetumika kwa ajili ya kutoa zawadi za kuwawezesha watu wenye mahitaji maalum kufurahia sikukuu zijazo, na mahitaji hayo yanajumuisha vyakula pamoja na vinywaji," alisema Dkt. Dorothy.


Alisema mbali na msaada wa vyakula, Rais Samia alitoa vifaa mbalimbali kwa lengo la kuwaendeleza watoto na kuimarisha huduma katika makao ya watoto, ikiwa ni pamoja na vifaa vya shule, majiko, mashine za kufulia, majokofu, na vifaa vingine vya kazi. Jumla ya vituo 153 vya Tanzania Bara na Zanzibar vilinufaika na msaada huo.


Mkurugenzi wa Kituo cha Yatima cha Amani kilichopo Kigamboni, Hajjaty Zubeida Abdallah, alisema zawadi hizo ni faraja kwao, kwani kulea na kusimamia vituo hivyo ni kuisaidia serikali.


"Tunamshukuru Rais Samia kwa kutambua mchango wetu, kwani tunapolea makundi haya, ni dhahiri tunasaidia serikali kwa kuwapa malezi bora, elimu, na mengine ambayo baadaye yanasaidia jamii kuleta maendeleo," alisema Zubeida.


Naye Ofisa Ustawi wa Jamii wa Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu, Juma Samora, aliishukuru serikali kwa kuwakumbuka watu wenye ulemavu, kwani inawatia moyo na kuona wanathaminiwa.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.