Bi. Jane Kalimasi, muuguzi mstaafu na mwanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ametoa shukrani zake za dhati kwa Mungu, akimshukuru kwa kumwezesha kulitumikia taifa kwa uaminifu na hatimaye kustaafu salama. Akiwa na miaka mitano tangu alipostaafu, Bi. Kalimasi ameelezea kuridhishwa kwake na huduma bora anazoendelea kupata kutoka PSSSF, kauli aliyoitoa wakati wa semina maalum iliyoandaliwa na mfuko huo kwa ajili ya wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Mwanza.
"Nilimuomba Mungu nifikishe umri wa miaka 55 salama, na kwa neema yake, ombi langu lilitimia. Nikaamua kustaafu mwaka 2019, na sasa nina miaka mitano tangu nistaafu," alisema Bi. Kalimasi. Alisisitiza kuwa anashukuru sana kwa kuwa mafao yake ya kustaafu yalilipwa ndani ya muda uliowekwa kisheria, na pensheni yake ya kila mwezi inalipwa kwa wakati bila kuchelewa. Hali hii imemwezesha kuendelea na maisha yake ya kistaafu kwa utulivu na bila changamoto za kifedha.
Bi. Kalimasi alifafanua kuwa kwa sasa, huduma zinazotolewa na PSSSF zimeboreshwa sana, akibainisha kuwa wanachama wanapofika katika ofisi za mfuko huo, wanapata huduma bora na za haraka sana. "Vitu ambavyo navipenda zaidi kutoka PSSSF katika kipindi chote cha ustaafu wangu ni pamoja na huduma ya PSSSF kidijitali kupitia simu yangu ya mkononi. Ninatumia App yao kupata taarifa zote muhimu. Pia, ninapokea ujumbe kwenye simu yangu punde tu pensheni yangu inapoingizwa kwenye akaunti yangu, jambo linalonipa uhakika na amani ya moyo," alieleza.
"Na kubwa zaidi, kwa kuwa mimi ni mwanachama wa PSSSF, ninaweza kukopa fedha kutoka benki chini ya udhamini wa PSSSF. Hakika hizi ni huduma bora kabisa zinazotuwezesha sisi wastaafu kuendelea kujitegemea na kutimiza mahitaji yetu," aliongeza mstaafu huyo, akionesha jinsi mfuko unavyowawezesha wanachama wake hata baada ya kustaafu. Uwezo wa kukopa chini ya udhamini wa PSSSF ni fursa adhimu inayowapa wastaafu uwezo wa kifedha wa kutekeleza mipango yao mbalimbali, kama vile kuanzisha biashara ndogo ndogo au kuboresha maisha.
Akizungumza katika semina hiyo, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Mwanza, Edwin Soko, alitoa shukrani za dhati kwa PSSSF kwa mchango wao katika masuala mbalimbali ya klabu hiyo, ikiwemo kuandaa semina hii muhimu ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuuelewa vizuri mfuko huo. "Tunawashukuru sana PSSSF kwa kuja kutuelimisha. Maarifa haya yatatusaidia kuandika habari sahihi na zenye tija kwa jamii," alisema Bw. Soko.
Bw. Soko aliwataka waandishi wa habari kutumia fursa hiyo kujifunza na kuandika habari zenye kutoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili wananchi, na kusaidia taasisi kama PSSSF ambazo zina jukumu muhimu la kutoa huduma kwa jamii. Semina hiyo ya siku moja, iliyoandaliwa na PSSSF kwa wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Mwanza, ni sehemu ya mkakati wa mfuko huo kukutana na wadau mbalimbali ili kuwajengea uelewa mpana kuhusu majukumu na huduma zake, huku wakipokea maoni na ushauri kutoka kwa umma.