Mafanikio ya Wanawake Iran: Mfano wa Kuigwa Tanzania katika Elimu, Uongozi na Afya

culture | Tue Feb 11 2025


Mafanikio ya Wanawake Iran: Mfano wa Kuigwa Tanzania katika Elimu, Uongozi na Afya

Kituo cha Kiislamu cha Hazrat Masoomeh kilichopo Dar es Salaam, Tanzania, kimefanya mkutano muhimu wa kisayansi na kitamaduni kwa lengo la kuwaelimisha wanafunzi kuhusu mafanikio yaliyopatikana kupitia Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, hususan katika kuimarisha nafasi na haki za wanawake katika jamii. Mkutano huo, uliokuwa na mada "Kujifunza Kuhusu Mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu katika Nyanja ya Wanawake," ulilenga kuonyesha mchango mkubwa wa mapinduzi hayo katika kuleta usawa wa kijinsia na maendeleo ya wanawake.


Dkt. Mohsen Maarefi, Mkurugenzi wa Kituo cha Utamaduni cha Iran, alieleza kuwa wanawake walikuwa mstari wa mbele katika harakati za kuleta Mapinduzi ya Kiislamu, wakishiriki kwa wingi hata kabla ya wanaume. Alifafanua kuwa mapinduzi hayo yameleta mabadiliko chanya kwa wanawake wa Iran katika sekta mbalimbali muhimu kama elimu, uongozi, na ushiriki katika shughuli za kijamii, hatua ambazo zimeongeza kwa kiasi kikubwa usawa wa kijinsia nchini humo.


Akitoa takwimu mbalimbali, Dkt. Maarefi alisema kuwa mafanikio makubwa yameonekana katika elimu, ambapo asilimia 33.3 ya wanafunzi wote wa vyuo vikuu nchini Iran ni wanawake. Zaidi ya hayo, idadi ya wanawake wanaojiunga na vyuo vikuu vya matibabu imefikia asilimia 34. Aliongeza kuwa juhudi za mapinduzi zimewezesha kupunguza sana tatizo la ujinga miongoni mwa wanawake kwa asilimia kubwa ya 99.3.


Takwimu zaidi zinaonyesha kuwa uwiano wa wanafunzi wa kike na wa kiume katika ngazi mbalimbali za elimu umeongezeka kwa asilimia 28. Uandikishaji wa wanawake katika vyuo vikuu umeongezeka kwa asilimia 56. Katika ujasiriamali, idadi ya wanawake wajasiriamali imeongezeka hadi kufikia asilimia 24, na zaidi ya wanawake 4,000 wanamiliki na kuendesha biashara zao wenyewe nchini Iran.


Katika sekta ya michezo, kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya gym (kumbi za mazoezi) kwa wanawake, ambapo zimeongezeka mara 30. Wanawake wanamichezo wa Iran wamefanikiwa kupata medali 3,302 katika mashindano ya kimataifa. Pia, kuna ongezeko kubwa la wanawake wanaoshiriki kama waamuzi katika mashindano ya michezo, ambapo wameweza kufikia idadi ya marefa 88,366 wanaoshiriki katika mashindano ya ndani na kimataifa. Wanawake wamepata pia nafasi 97 katika Shirikisho la Kimataifa la Michezo.


Sekta ya habari na filamu pia imeshuhudia ushiriki mkubwa wa wanawake. Kuna zaidi ya waandishi wa habari wanawake 840 na waandishi wengine wanawake 9,500 ambao wanachangia kwa kiasi kikubwa katika vyombo vya habari nchini Iran. Katika tasnia ya filamu, waandaaji wa filamu wanawake wameshinda tuzo 128 za kimataifa na 114 za kitaifa, huku wanawake 903 wakishiriki moja kwa moja katika utengenezaji wa filamu.


Dkt. Maarefi aligusia pia mafanikio makubwa katika sekta ya afya. Zaidi ya asilimia 95 ya wajawazito wanajifungua chini ya uangalizi wa wataalamu wa uzazi. Idadi ya madaktari wanawake wataalamu imeongezeka kwa kasi kutoka 597 hadi 30,000. Aidha, wastani wa maisha ya wanawake nchini Iran umeongezeka kutoka miaka 54 hadi 78. Iran inashika nafasi ya 10 duniani kwa kuwa na kiwango cha chini cha vifo vinavyosababishwa na saratani ya shingo ya kizazi.


Bi. Munireh Haitham Tajari, mkuu wa shule ya Hazrat Masoomeh, alisema kuwa mafanikio haya ya Mapinduzi ya Kiislamu, hasa katika kuwawezesha wanawake, ni mfano mzuri wa kuigwa na wasichana na wanawake wa Tanzania. Aliongeza kuwa kujifunza kutoka kwa mifano halisi kama hii huwasaidia wanawake kutambua fursa zilizopo kwao kushiriki kikamilifu katika jamii na kufikia malengo yao.


Bi. Hidaya Idrisa, mmoja wa wanafunzi walioshiriki mkutano huo, alisisitiza kuwa uhamasishaji kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii unapaswa kuanzia ngazi ya familia kwa kuwaelimisha wazazi. Bi. Zawia Juma aliwahamasisha wanawake wenzake wasikate tamaa katika harakati zao za maendeleo na badala yake washirikiane kupitia jumuiya za wanawake na kutafuta msaada kutoka serikalini ili kufanikisha ndoto zao.


Mkutano huu ulikuwa fursa muhimu kwa wanafunzi wa Tanzania kujifunza kuhusu mchango wa wanawake katika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kupata motisha ya kuendelea kutafuta njia za kujikomboa na kujenga maisha bora kwao na kwa jamii zao.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.