Kishimba Awashirikisha Walimu Kugawana Milioni 77 za Mfuko wa Jimbo

culture | Thu Apr 03 2025


Kishimba Awashirikisha Walimu Kugawana Milioni 77 za Mfuko wa Jimbo

Mbunge wa Jimbo la Kahama, Jumanne Kishimba, amefanya mkutano na walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari wa Manispaa ya Kahama ili kuwashirikisha namna ya kugawanya fedha za mfuko wa jimbo, kiasi cha shilingi milioni 77, kwa lengo la kuboresha mazingira ya shule zao.


Kishimba aliongoza mkutano huo katika ukumbi wa manispaa ya Kahama, ambapo walijadili na kupata mapendekezo ya matumizi ya fedha hizo. Walimu walieleza mahitaji yao mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ujenzi na ukamilishaji wa vyumba vya madarasa, pamoja na ujenzi wa vyoo kwa ajili ya walimu na wanafunzi.


Kishimba alisema kuwa kila anapopokea fedha za jimbo kila mwaka, amekuwa akishirikisha idara zote muhimu, hasa za elimu na afya, ili kuangalia namna bora ya kuzigawa fedha hizo. Lengo lake ni kutatua changamoto mbalimbali, kuboresha miundombinu, na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma katika mazingira mazuri.


"Nimepokea fedha kiasi cha shilingi milioni 77, na ndiyo sababu ya kuwaita walimu wakuu wa shule za msingi, sekondari na wenyeviti wa mitaa, ili kuwasilisha changamoto zinazowakabili shuleni. Fedha hizi zitagawanywa na kila mmoja atazitumia kuboresha mazingira ya shule yake," alisema Kishimba.


Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mbulu B, Rehema Magege, alieleza kuwa shule yake ina zaidi ya wanafunzi 1,275, kuanzia darasa la awali hadi la saba. Wanafunzi hao wanatumia matundu nane tu ya vyoo, ambapo manne yanatumiwa na wanafunzi wa kiume (582) na mengine manne yanatumiwa na wanafunzi wa kike (693).


Magege aliongeza kuwa walimu wanashirikiana na wanafunzi katika kutumia vyoo hivyo, na aliomba sehemu ya fedha hizo zitumike kujenga angalau vyoo kwa ajili ya walimu. Alisema kuwa upungufu wa matundu ya vyoo kwa wanafunzi ni 52.


Mwalimu wa Shule ya Msingi Mayila, Japhet Ngulu, alisema kuwa shule yake ina wanafunzi 1,895, lakini ina vyumba vya madarasa 14 tu kati ya 42 vinavyohitajika. Hii ina maana kuwa shule hiyo ina upungufu wa madarasa 28. Ngulu aliomba kupatiwa tofali 2,000 ili kuanza ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa.


Ngulu alieleza kuwa darasa moja katika shule yake linabeba wanafunzi zaidi ya 180, hali ambayo inafanya iwe vigumu kwa walimu kusahihisha mazoezi ya wanafunzi. Aliongeza kuwa kila mwaka shule hiyo inapokea zaidi ya wanafunzi 500, idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na idadi ya madarasa yaliyopo.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.