Kata ya Tuwemacho, iliyoko katika wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, imeshuhudia mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika sekta mbalimbali, yaliyowezekana kutokana na uwekezaji mkubwa wa serikali katika miradi ya kijamii. Kulingana na Diwani wa kata hiyo, Mhe. Hadija Timamu, hatua hizi zimeifanya Tuwemacho kupiga hatua kubwa zaidi za maendeleo kuliko wakati wowote tangu Tanzania ipate uhuru wake mwaka 1961.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kata hiyo, Diwani Timamu alieleza kuwa katika kipindi cha miaka minne tangu kuanza kutekelezwa kwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020, serikali imefanya kazi kubwa katika kujenga na kuboresha miundombinu muhimu katika sekta za elimu, afya, maji, na barabara.
Katika sekta ya maji, Mhe. Timamu alifafanua kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 pekee, kata ya Tuwemacho imepokea miradi miwili muhimu ya maji. Mradi mmoja unatekelezwa katika Kijiji cha Tuwemacho na mwingine katika Kijiji cha Namasalau, hususan katika kitongoji cha Mdingula. Aliongeza kuwa mradi mkuu wa maji, wenye thamani ya takribani TZS 1,054,232,603.55 (shilingi bilioni moja, milioni hamsini na nne, laki mbili thelathini na mbili, na mia sita tatu na senti hamsini na tano), ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia wakazi wa vijiji vya Tuwemacho, Namasalau, Nasya, Chemchem, na baadhi ya vitongoji vingine ndani ya kata hiyo. Aidha, mradi mwingine mdogo katika Kijiji cha Namasalau, eneo la Mdingula, unatekelezwa kwa gharama ya TZS milioni 60.1 (shilingi milioni sitini na laki moja).
Katika sekta ya elimu, serikali imejenga shule mpya ya sekondari katika Kata ya Tuwemacho kwa gharama ya awali ya TZS milioni 560 (shilingi milioni mia tano na sitini). Shule hii inatarajiwa kuwa na wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita. Hata hivyo, kutokana na kuongezwa kwa majengo ya madarasa na mabweni, gharama ya mradi imefikia TZS 1,075,552,825 (shilingi bilioni moja, milioni sabini na tano, laki tano hamsini na mbili, na mia nane ishirini na tano). Mhe. Timamu alisema kuwa shule hii imepunguza sana adha waliyokuwa nayo wanafunzi wa kusafiri umbali mrefu kutafuta elimu ya sekondari katika kata zingine. Aliongeza kuwa uwepo wa shule hiyo umeongeza hamasa ya watoto kupenda masomo, tofauti na hapo awali ambapo wengi walikuwa wanaishia elimu ya msingi (darasa la saba). Diwani Timamu pia alibainisha kuwa serikali imejenga vyumba viwili vya madarasa katika Kijiji cha Namasalau kwa gharama ya TZS milioni 30 (shilingi milioni thelathini), pamoja na ujenzi wa matundu 18 ya vyoo katika Shule ya Msingi Namasalau kwa gharama ya TZS 42,871,045.41 (shilingi milioni arobaini na mbili, laki nane sabini na moja, na arobaini na tano na senti arobaini na moja).
Akizungumzia kuhusu sekta ya afya, Diwani Timamu alisema kuwa hadi mwaka 2020, kata ya Tuwemacho ilikuwa na zahanati moja tu iliyoko katika Kijiji cha Tuwemacho, ambayo ilijengwa kupitia mradi wa TASAF (Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania). Wananchi kutoka vijiji vingine walilazimika kutembea umbali mrefu hadi kufikia kilomita 12 ili kupata huduma za afya. Hivi sasa, kata hiyo inajivunia kuwa na zahanati tatu zilizokamilika katika vijiji vya Tuwemacho, Namasalau (iliyokamilika mwaka 2020), na Nasya (iliyokamilika mwaka 2023). Ingawa Kijiji cha Chemchem bado hakina kituo cha afya, mipango ya ujenzi wake tayari imeanza. Zahanati hizo zilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi wenyewe, lakini zilikamilishwa kwa msaada wa Mbunge wa jimbo hilo, Mhe. Daimu Mpakate, ambaye alitoa TZS milioni 16 (shilingi milioni kumi na sita) kupitia Mfuko wa Jimbo. Serikali pia ilichangia TZS milioni 50 (shilingi milioni hamsini) kwa kila zahanati kwa ajili ya ukamilishaji wake.
Katika eneo la miundombinu ya barabara, Mhe. Timamu alisema kuwa kata hiyo imefaidika na miradi ya ufunguzi, ukarabati, na uboreshaji wa barabara mbalimbali. Lengo la miradi hii ni kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao kutoka maeneo ya vijijini hadi kwenye masoko.
Baadhi ya wananchi wa Tuwemacho, akiwemo Mwanabibi Mussa na Bwana Said Juma, walitoa shukrani zao kwa serikali kwa kutekeleza miradi hiyo. Walieleza kuwa kata yao imeanza kufunguka kiuchumi na kijamii kutokana na maboresho hayo. Kwa upande wake, Mwalimu Teresia Ng’ombo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Tuwemacho, alisema kuwa shule hiyo kwa sasa ina wanafunzi 188 wa kidato cha kwanza na cha pili, ina walimu 10, na inatoa michepuo ya masomo ya sayansi na sanaa. Alibainisha kuwa mwezi Julai mwaka huu, wanatarajia kupokea wanafunzi wa kike watakaoanza kidato cha tano. Wanafunzi wa shule hiyo – Twaibu Hashimu, Rehema Alai, na Ismail Rashid – walieleza kuwa shule yao ina mazingira mazuri ya kujifunzia na ina walimu wa kutosha. Walisema kuwa ujio wa wanafunzi wa kidato cha tano na sita utawasaidia kuongeza motisha ya kusoma na kuimarisha ushindani wa kitaaluma shuleni.