Wakati dunia ikielekea kuadhimisha Siku ya Watu Wenye Ulemavu hapo kesho, kengele ya hatari imepigwa kutoka katika viunga vya Mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro. Imebainika kuwa kundi la watoto wanaozaliwa na changamoto ya Kichwa Kikubwa (Hydrocephalus) na Mgongo Wazi (Spina Bifida) nchini, linaelekea kusahaulika kabisa katika 'kapu' la bajeti ya serikali, huku maelfu wakipoteza maisha au kupata ulemavu wa kudumu kutokana na ukosefu wa huduma maalum.
Hayo yameibuliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Child-Help International (Tanzania), Bi. Janeth Manoni, wakati akizungumza na waandishi wa habari jana, Desemba 1, 2025. Bi. Manoni ameweka bayana takwimu zinazotisha, akieleza kuwa kila mwaka, Tanzania inapokea watoto wapya 7,500 wenye changamoto hizo, idadi ambayo ni kubwa na inahitaji mkakati wa kitaifa.
"Wenzetu Wanaonekana, Sisi Tumesahaulika" Bi. Manoni amepaza sauti kwa uchungu, akidai kuwa licha ya serikali kujitahidi kwenye sekta ya afya, kundi hili maalum limeachwa yatima. "Tunapoadhimisha siku hii tarehe 3 Desemba, tuna ujumbe mzito na mahususi kwa serikali. Tunataka wajue kuwa hawa watoto wapo na wanateseka. Katika aina mbalimbali za ulemavu, utasikia zikijadiliwa na kutengewa fungu, lakini ukija kwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi, ni kimya kingi," alilalamika Mkurugenzi huyo.
Kilio hicho kinalenga kuamsha mamlaka husika kuweka kipaumbele cha kibajeti ili kuokoa maisha ya watoto hawa ambao wengi wao huzaliwa katika familia zisizo na uwezo wa kumudu gharama za matibabu na vifaa tiba.
Moshi Kuweka Historia Duniani Hata hivyo, katikati ya changamoto hizo, Mkoa wa Kilimanjaro unatarajia kuandika historia mpya duniani. Bi. Manoni ametangaza kuwa Desemba 3, 2025, itakuwa siku ya uzinduzi wa Nyumba ya Maarifa (Share Knowledge Center) mjini Moshi. Kituo hiki kinatajwa kuwa ni cha kwanza cha aina yake kuwahi kuanzishwa duniani kote, kikiwa na lengo la kuwa kisima cha elimu na taarifa sahihi kuhusu matatizo hayo.
Mwasisi na Rais wa Shirika la Child-Help International, Bw. Pierre Mertens, amefafanua kuwa adui mkubwa anayeua watoto hawa si ugonjwa wenyewe, bali ni ujinga. "Watoto wengi wanakufa si kwa sababu hawatibiki, la hasha! Wanakufa kwa sababu maarifa sahihi hayawafikii wazazi na walezi kwa wakati. Kituo hiki cha Moshi kitakuwa mkombozi wa kutoa elimu hiyo," alisisitiza Mertens.
Huduma Bora si Mashine, ni Utu Naye Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu kwa watoto, Dk. Carla Verpoorten, ametoa angalizo la kitabibu. Amesema kuwa jamii imekuwa ikiamini kuwa kuokoa watoto hawa kunahitaji mashine za mabilioni, jambo ambalo si kweli kabisa.
"Kinachookoa maisha ya mtoto mwenye mgongo wazi si teknolojia ya angani. Siri ni ufuatiliaji wa karibu (continuity of care), usafi wa vidonda, mpangilio sahihi wa mwili na lishe bora. Haya yakizingatiwa, mtoto anaweza kuishi maisha marefu na yenye furaha," alifafanua Dk. Verpoorten.
Uzinduzi wa kituo hicho unatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko, huku wadau wakisubiri kuona kama serikali itaitikia wito wa kuwatengea bajeti maalum watoto hawa katika mwaka ujao wa fedha.