Kwa wakazi 3,852 wa Kijiji cha Makuro wilayani Singida, adha ya kuamka alfajiri na kutembea umbali wa kilomita tisa kuwania maji machafu kwenye makorongo yaliyokuwa yakitumiwa pia na wanyama wakali kama fisi, sasa imebaki kuwa historia. Hii ni baada ya serikali, kupitia Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), kufanikisha mradi kabambe wa maji safi na salama wenye thamani ya Shilingi milioni 724.
Hali ya maisha kabla ya mradi huu ilikuwa ya hatari na kero kubwa, kama alivyoeleza mmoja wa wakazi, Mwanahamisi Salum. "Ilikuwa ni mapambano ya kweli. Unakwenda korongoni kuchota maji, huku unahofia kukutana na fisi. Mradi huu si tu umetuletea maji, bali umerejesha utu na hata amani kwenye ndoa zetu, kwani ule msongo wa mawazo wa kufuata maji umekwisha," alisema.
Akizungumzia mafanikio hayo, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Singida, Lucas Said, alibainisha kuwa mradi huu umechangia kupandisha kiwango cha upatikanaji wa maji katika wilaya ya Singida hadi kufikia asilimia 80.3. Aliongeza kuwa mkakati wa mkoa ni kuhakikisha huduma inafikia asilimia 78.5 kwa vijiji vyote ifikapo mwisho wa mwaka huu, kutoka asilimia 71.3 ya sasa.
Wakati akizindua rasmi mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, aliwasihi wananchi kuwa walinzi wa kwanza wa miundombinu hiyo ili iweze kudumu na kuhudumia vizazi vijavyo. Katika hatua inayoonesha serikali inathamini mchango wa raia, Bi. Dendego aliiagiza RUWASA kumlipa fidia ya Shilingi 500,000 mwananchi aliyejitolea ardhi yake kwa ajili ya ujenzi wa kisima kikuu cha mradi. Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya, Godwin Gondwe, alithibitisha kuwa serikali iko macho, kwani tayari kero zaidi ya 200 za maji zimepokelewa na kutatuliwa wilayani humo.