Wakati Tanzania ikiungana na ulimwengu kuadhimisha Siku ya Usafiri Majini Duniani leo Septemba 26, Shirika la Uwaka la Meli Tanzania (TASAC) limetoa wito mzito kwa jamii, likisisitiza umuhimu wa kuwianisha matumizi ya rasilimali za bahari na jukumu la kuyalinda mazingira yake kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Akizungumza katika taarifa yake, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salum, alisema kaulimbiu ya mwaka huu, “Bahari Yetu, Wajibu Wetu, Fursa Yetu,” inatumika kama kumbusho kwamba bahari ni uhai na ni nguzo ya uchumi, lakini inakabiliwa na tishio kubwa kutokana na shughuli za binadamu. Alieleza kuwa bahari ndiyo chanzo cha zaidi ya asilimia 60 ya hewa ya oksijeni tunayovuta na inafyonza kiasi kikubwa cha hewa ya ukaa, na hivyo kusaidia kupunguza kasi ya mabadiliko ya tabianchi.
"Tangu zamani, bahari imekuwa njia kuu ya biashara inayounganisha dunia, na chanzo cha mamilioni ya ajira kupitia uvuvi, utalii, na usafirishaji. Hata hivyo, tunapaswa kutambua kuwa uwezo huu wa bahari kutoa fursa za kiuchumi unategemea afya yake," alisema Bw. Salum.
Alionya kuwa uchafuzi mkubwa unaotokana na plastiki, kemikali za viwandani, uvuvi haramu, na umwagikaji wa mafuta umeathiri vibaya mifumo ikolojia ya bahari. Alisisitiza kuwa uzalishaji mkubwa wa hewa ya ukaa hausababishi tu ongezeko la joto duniani na kupanda kwa kina cha maji, bali pia unaongeza tindikali baharini, hali inayohatarisha maisha ya viumbe kama matumbawe.
Kwa mantiki hiyo, TASAC imetoa wito kwa serikali, jamii, na watu binafsi kuchukua hatua za pamoja. Hii ni pamoja na kuunga mkono usafirishaji endelevu, kupunguza matumizi ya plastiki, na kuhamasisha mabadiliko ya sera yatakayohakikisha ulinzi wa bahari.
"Adhimisho hili ni fursa ya sisi sote kutafakari na kuchukua hatua. Ni lazima tuendeleze fursa za uchumi wa buluu, lakini kwa njia endelevu inayohakikisha tunailinda na kuithamini bahari yetu kama tunavyothamini maisha yetu," alihitimisha.