Mvutano unaoendelea kuhusiana na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, umechukua sura mpya baada ya Jeshi la Polisi nchini kutangaza rasmi kuwa limefungua jalada la uchunguzi dhidi ya tuhuma nzito ambazo mwanasiasa huyo amekuwa akizitoa. Aidha, jeshi hilo limemtaka Balozi Polepole kufika mara moja katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa ajili ya mahojiano.
Katika taarifa yake rasmi kwa umma, Jeshi la Polisi limeeleza kuwa limekuwa likifuatilia kwa karibu madai mbalimbali ambayo Balozi Polepole amekuwa akiyaeneza kupitia mitandao ya kijamii tangu alipojiuzulu wadhifa wake mwezi Julai, 2025. Kwa mujibu wa jeshi hilo, baadhi ya tuhuma hizo zina viashiria vya kutendeka kwa makosa ya kijinai, ambayo kwa mujibu wa sheria za nchi, yanahitaji uchunguzi wa kina na uthibitisho wa kisheria.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa, kama sehemu ya mchakato wa uchunguzi, Jeshi la Polisi limekuwa likikusanya taarifa na ushahidi kuhusiana na madai hayo. Hata hivyo, imeelezwa kuwa jitihada za awali za kumpata Balozi Polepole ili aweze kutoa maelezo rasmi na kuwasilisha vielelezo vyake hazijafanikiwa.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi limetoa agizo rasmi likimtaka Balozi Polepole kuripoti kwa DCI ili aeleze kwa undani kuhusu tuhuma anazozitoa, hatua ambayo itawezesha upelelezi kukamilika na hatua nyingine za kisheria kuweza kuchukuliwa. Taarifa ya polisi imesisitiza umuhimu wa ushirikiano wake katika kufanikisha uchunguzi huu ili haki iweze kutendeka.