Fatma Ally, mmoja wa wanawake wachache nchini Tanzania wanaofanya kazi kama kondakta katika mabasi ya kampuni ya Tilisho Safaris, ametoa wito maalum kwa wasichana na wanawake wote nchini kuondokana na dhana potofu na mtazamo hasi walionao kuhusu kazi hiyo. Amewataka kutambua kuwa ukondakta ni ajira halali na kama kazi nyingine yoyote, inaweza kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika maisha yao.
Katika mahojiano yake ya kipekee na Nipashe Digital, Fatma alielezea kwa ujasiri jinsi kazi hii ya ukondakta imemwezesha kujipatia kipato kinachomsaidia kukidhi mahitaji yake ya kimsingi na kulea familia yake kwa uhuru.
"Ukondakta ni kazi kama kazi nyingine, ni ajira rasmi ambayo imetambuliwa na serikali. Kupitia kazi hii, nimebahatika kukutana na watu mbalimbali ambao wamekuwa na mchango mkubwa na tija katika maisha yangu," alisema Fatma kwa kujiamini.
Akifafanua zaidi, Fatma alieleza kuwa kazi ya ukondakta imempa uhuru wa kifedha na kumwezesha kujitegemea katika kuyamudu mahitaji yake muhimu bila kuwa tegemezi.
"Kazi hii inanifanya niwe nadhifu na msikivu muda wote, inanipa kipato kinachonitosha kujikimu kimaisha, na zaidi ya yote, ninajivunia sana kutoa huduma kwa jamii. Kuwahudumia abiria mbalimbali kunanifanya nihisi ubinadamu wangu na kuona upendo kutoka kwao," aliongeza Fatma kwa furaha.
Fatma anafanya kazi katika mabasi yanayosafirisha abiria kutoka jiji la Dar es Salaam kuelekea miji ya Arusha na Rombo. Katika safari zake, ameendelea kuwaelimisha na kuwahamasisha wasichana wengine kujitokeza na kutafuta fursa mbalimbali za ajira badala ya kujifungia kwenye mitazamo hasi isiyo na msingi kuhusu kazi fulani.
Kupitia mfano wake halisi, Fatma anathibitisha kuwa kazi yoyote ile inayompatia mtu kipato halali ni heshima na inastahili kuthaminiwa. Anawashauri wanawake kuwa wanaweza kufanya kazi katika sekta mbalimbali bila ya kuwa na hofu au kujiona duni, kwani uwezo wao ni sawa na wa wanaume katika kufanya kazi yoyote ile mradi wawe na nia, bidii, na kujituma.