Wakati klabu ya Yanga ikijiandaa kwa mtanange wao muhimu wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers nchini Malawi, vita ya kimbinu imeanza hata kabla ya mpira kupigwa. Uongozi wa mabingwa hao wa Tanzania umefichua kuwa wamegundua silaha ya ziada ya wapinzani wao – hali ya hewa ya joto kali inayotarajiwa kuwepo kwenye Uwanja wa Bingu Mutharika, Lilongwe, siku ya Jumamosi.
Akifafanua mkakati wa timu hiyo, Afisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alieleza kuwa baada ya kufanya upelelezi wa kina kuhusu wapinzani wao, walibaini kuwa mchezo huo utapigwa majira ya saa tisa alasiri kwa saa za Malawi (saa kumi kwa Tanzania), muda ambao jua huwa linawaka vikali. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Yanga waliamua kwa makusudi kucheza mchezo wao wa kirafiki dhidi ya TRA United Ijumaa iliyopita wakati wa mchana kweupe.
"Wengi waliona matokeo ya suluhu dhidi ya TRA United, lakini lengo letu halikuwa kwenye magoli. Dhamira yetu kuu ilikuwa ni kuwaandaa wachezaji wetu kuzoea mazingira magumu ya kucheza kwenye joto kali. Tulitaka miili yao ianze kuzoea hali hiyo ili tutakapofika Malawi, kisu hicho cha joto kisiwe na makali kwetu," alifafanua Kamwe. Alisema mkakati huo ulikubaliwa na TRA United na umewapa Yanga uhakika wa kwenda kupambana bila kusumbuliwa na hali ya hewa.
Wakati timu ikijiandaa kiufundi, nguvu ya mchezaji wa kumi na mbili haijaachwa nyuma. Kamwe aliwasifu na kuwapongeza wanachama na mashabiki wa Yanga, hasa kutoka mikoa ya nyanda za juu kusini kama Mbeya na Iringa, kwa kuonyesha mwamko wa hali ya juu wa kujipanga kusafiri hadi Malawi kuipa timu sapoti. "Mwamko ni mkubwa sana, hasa kwa wenzetu wa Mbeya na Iringa ambao wako jirani. Hata hapa Dar es Salaam watu wanajiorodhesha. Tunawasihi Wanayanga wajitokeze kwa wingi, imebaki hatua moja tu tufike kwenye hatua ya makundi," alihimiza.
Baada ya mchezo wa Jumamosi nchini Malawi, pambano la marudiano linatarajiwa kupigwa Oktoba 25 katika dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Yanga waliingia raundi hii baada ya kuifunga Wiliete du Benguela ya Angola kwa jumla ya mabao 5-0.