Hivi karibuni, kauli iliyotolewa na wakala wa kiungo mahiri wa Liverpool, Ryan Gravenberch, ilizua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka, hali iliyomlazimu wakala huyo kujitokeza na kufafanua mambo ili kutuliza hali. Taarifa kutoka chombo cha habari cha Uingereza, 'Talk Sport', zimethibitisha kuwa wakala huyo, Jose Fortes Rodriguez, amekanusha vikali tetesi kwamba mchezaji wake anawazia kuhamia Real Madrid.
Gravenberch, ambaye ni zao la akademi maarufu ya Ajax, alihamia Bayern Munich mnamo Julai 2022. Akiwa na miamba hao wa Ujerumani, alicheza michezo 33, ingawa mingi aliingia akitokea benchi. Msimu uliofuata, alitua Liverpool ambapo katika msimu wa 2023-24, alishiriki katika michezo 38, akipangwa kuanza na wakati mwingine kuingia kama mchezaji wa akiba.
Hata hivyo, msimu huu wa sasa, Gravenberch ameimarika na kuwa mmoja wa wachezaji tegemeo katika kikosi cha Liverpool. Amecheza jumla ya mechi 43 katika mashindano yote rasmi, na cha kufurahisha zaidi kwa mashabiki wa Liverpool, alianza katika kila mchezo. Ametengeneza kombinesheni imara katika safu ya kiungo pamoja na wachezaji wengine kama Alexis Mac Allister na Dominik Szoboszlai, akitoa mchango mkubwa katika mbio za timu hiyo kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (PL), ambapo kwa sasa wanaongoza ligi.
Wakati mchezaji huyo akiendelea kung'ara uwanjani, ndipo wakala wake, Jose Fortes Rodriguez, alipotoa kauli iliyoibua hisia kali. Kulingana na 'Talk Sport', Rodriguez alifanya mahojiano na gazeti la Hispania, 'Marca', na kusema kuwa angetamani siku moja kumwona Gravenberch akivaa jezi ya Real Madrid. Kauli hii iligusa hisia za mashabiki wa Liverpool ambao tayari wapo kwenye taharuki kutokana na uvumi unaomhusisha beki wao wa kulia na kipenzi chao, Trent Alexander-Arnold, pamoja na beki wa kati Ibrahima Konaté, kuhamia Real Madrid. Inadaiwa Alexander-Arnold, ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, tayari amefanya mazungumzo ya awali na Real Madrid.
Rodriguez alinukuliwa akisema, "Wakati Gravenberch alipokuwa na miaka 16, Barcelona walionyesha nia ya kumsajili. Lakini mimi na baba yake tulichagua Ajax badala ya Barcelona kwa sababu tuliamini Ajax ingempa fursa bora ya kukua kimchezo kwa utaratibu mzuri." Aliendelea, "Ana uwezo wa kucheza Real Madrid. Tunatamani angecheza huko."
Maneno haya hayakupokelewa vizuri na mashabiki wa Liverpool. Kutokana na hali hiyo, Rodriguez alitumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kujaribu kurekebisha hali. Alieleza, "Mimi ni Mhispania, na Real Madrid ni klabu ya ndoto yangu binafsi. Lakini si klabu ya ndoto ya Gravenberch. Ryan ana furaha kubwa sana kuwa Liverpool. Ukimwuliza yeye mwenyewe, atakuambia Liverpool ndiyo klabu bora zaidi duniani." Ufafanuzi huu unalenga kuwahakikishia mashabiki wa Liverpool kuwa mchezaji wao bado ana mapenzi na klabu hiyo na hana mpango wa kuondoka kwa sasa.