Kinyang'anyiro cha urais nchini kimeingia katika sura mpya ya mivutano ya kisheria na kisiasa, baada ya mgombea wa chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Mpina, kuzuiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kurejesha fomu zake za uteuzi jijini Dodoma. Tukio hili la kushangaza limetokea siku ileile ambayo mgombea wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, alikamilisha mchakato huo kwa shangwe na kuidhinishwa rasmi kuingia kwenye kinyang'anyiro.
Chama cha ACT Wazalendo kimepinga vikali hatua hiyo, kikiielezea kama hujuma na ukiukwaji wa haki ya kidemokrasia. Kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wake, Omari Said Shaaban, chama hicho kimeweka wazi kuwa kimelazimika kufungua kesi mahakamani kupinga kile walichokiita uamuzi usio wa haki wa INEC. Shaaban alifafanua kuwa Mpina alijiunga rasmi na chama hicho Julai 29, na kwa mujibu wa katiba yao inayohitaji mwanachama kukaa angalau siku saba kabla ya kugombea, alikuwa ametimiza vigezo vyote kufikia Agosti 4, tarehe ya kuchukua fomu.
"Tume yenyewe ilimpa fomu, ikahakiki wadhamini wake, kisha ikampa barua ya kumtaka arejeshe. Cha ajabu ni kuona tume hiyo hiyo inageuka na kumzuia baada ya kupokea barua kutoka kwa Msajili wa Vyama. Hii inakinzana wazi na Ibara ya 74 ya Katiba ya nchi inayosisitiza uhuru wa Tume," alisema Shaaban. Aliongeza kuwa ACT Wazalendo haitasimamisha mgombea mwingine na itaendelea kupambana kumtetea Mpina, wakiamini hawajavunja sheria yoyote.
Chanzo cha mkwamo huu kinatajwa kuwa ni barua ya malalamiko kutoka kwa mwanachama wao, MonaLisa Ndala, aliyepinga uhalali wa Mpina. Hata hivyo, chama kinadai kuwa kabla hawajajibu malalamiko hayo, mwanachama huyo alikimbilia kwa Msajili wa Vyama.
Wakati Mpina na viongozi wenzake wakikwama kwenye geti la ofisi za INEC jijini Dodoma, hali ilikuwa tofauti kabisa kwa Rais Samia. Yeye, akiwa ameambatana na mgombea mwenza wake Dk. Emmanuel Nchimbi na viongozi wa juu wa CCM, alirejesha fomu zake na kuidhinishwa rasmi na Mkurugenzi wa INEC, Ramadhan Kailima. Baada ya mchakato huo, Rais Samia alikabidhiwa gari jipya la kampeni aina ya Land Cruiser, kama ilivyo kwa wagombea wengine 16 ambao vyama vyao vimekamilisha mchakato huo bila vikwazo.