Mudryk Aishtakiwa kwa Kukiuka Sheria za Doping
Mshambuliaji wa Chelsea na timu ya taifa ya Ukraine, Mykhailo Mudryk, anakabiliwa na tishio la kufungiwa baada ya kutuhumiwa kukiuka kanuni za kupambana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli (doping).
Shirika la habari la Uingereza, BBC, limeripoti kuwa Chama cha Soka cha Uingereza (FA) kimeanzisha mchakato wa kuchunguza na kuamua adhabu inayofaa kutokana na madai ya Mudryk kukiuka sheria za doping. FA imesema: "Mudryk ameshitakiwa kwa tuhuma za kupatikana au kutumia dawa iliyopigwa marufuku. Kwa kuwa suala hili linaendelea, hatuwezi kutoa maoni zaidi."
Mudryk alisimamishwa kucheza kwa muda mnamo Desemba mwaka jana baada ya sampuli yake ya mkojo kupimwa na kuonyesha matokeo mabaya ya dawa ya Meldonium. Meldonium ni dutu inayojulikana kuongeza mtiririko wa damu na kuboresha utendaji wa kimichezo.
Mudryk amekanusha madai hayo akisisitiza kuwa "hakuwahi kutumia dawa iliyopigwa marufuku kwa makusudi," lakini amewekwa katika hatari ya kufungiwa kufuatia mashtaka ya FA.
Kulingana na kanuni za FA, ikiwa sampuli ya kwanza (A sample) itaonyesha matokeo mabaya, mchezaji ana haki ya kuomba uchunguzi wa sampuli ya pili (B sample). Ikiwa sampuli ya pili pia itaonyesha matokeo yale yale, basi mashtaka rasmi yatafuata.
BBC imeripoti kuwa mchezaji anayethibitishwa kutumia dawa iliyopigwa marufuku kwa makusudi anaweza kukabiliwa na kifungo cha hadi miaka minne, kwa mujibu wa miongozo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Mudryk alijiunga na Chelsea Januari 2023 akitokea Shakhtar Donetsk ya Ukraine, na mkataba wake na Chelsea unatarajiwa kuisha Juni 2031. Mudryk, ambaye ada yake ya uhamisho iliripotiwa kufikia hadi Pauni milioni 89 (takriban Shilingi bilioni 292 za Kitanzania), ameichezea Chelsea mechi 73 za mashindano na kufunga mabao 10.