Vigogo wa soka la Ujerumani, Bayern Munich, watalazimika kusubiri kidogo kabla ya kutawazwa rasmi kuwa mabingwa wa Bundesliga msimu wa 2024-25, baada ya kulazimishwa sare ya kusisimua ya mabao 3-3 na wenyeji wao RB Leipzig katika mchezo mkali uliopigwa kwenye dimba la Red Bull Arena.
Bayern Munich, wanaoongoza ligi kwa kishindo, walikuwa wanahitaji ushindi tu katika mchezo huu wa raundi ya 32 ili kujihakikishia taji lao la ligi bila kujali matokeo ya mechi zao mbili zilizosalia. Hata hivyo, bao la dakika za lala salama kutoka kwa Leipzig liliyeyusha matumaini hayo na kuwalazimu kusogeza mbele sherehe zao.
Hivi sasa, Bayern (pointi 76) wanaongoza ligi kwa tofauti ya pointi tisa dhidi ya Bayer Leverkusen (pointi 67) wanaoshika nafasi ya pili. Leverkusen bado wana michezo mitatu mkononi. Iwapo Leverkusen watashindwa kupata ushindi dhidi ya Freiburg katika mchezo wao ujao tarehe 5 Mei, basi Bayern watatangazwa kuwa mabingwa rasmi. Hata hivyo, ikiwa Leverkusen watashinda, Bayern watahitaji kupata angalau alama moja tu (sare) katika mchezo wao dhidi ya Borussia Mönchengladbach utakaopigwa tarehe 11 Mei ili kunyakua taji hilo.
Mchezo dhidi ya Leipzig ulikuwa na hekaheka za aina yake. Wenyeji Leipzig walianza kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya 11 kupitia kwa Benjamin Šeško. Mambo yakawa magumu zaidi kwa Bayern dakika ya 39 wakati Lukas Klostermann alipofunga bao la pili kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa na David Raum.
Wakiwa nyuma kwa mabao 2-0, Bayern walirejea kipindi cha pili kwa moto mkali. Dakika ya 62, beki wa kati Eric Dier alifunga bao la kwanza kwa kichwa akiunganisha kona iliyochongwa na Michael Olise. Dakika moja tu baadaye, Olise mwenyewe aligeuka kuwa mfungaji, akipokea pasi ya kichwa kutoka kwa Serge Gnabry na kufunga kwa shuti la mguu wa kushoto, na kuisawazishia Bayern.
Msisimko uliongezeka dakika ya 83 wakati winga wa Bayern, Leroy Sané, alipofunga bao la tatu kwa shuti kali la mguu wa kushoto, na kuwapa Bayern uongozi wa 3-2. Ilionekana kama taji lilikuwa linakwenda Munich. Hata hivyo, Leipzig hawakukata tamaa. Muda mfupi kabla ya filimbi ya mwisho, mshambuliaji wa Leipzig, Yussuf Poulsen, aliwanyamazisha mashabiki wa Bayern kwa kufunga bao zuri la kusawazisha kwa kuinua mpira juu ya kipa.
Mshambuliaji nyota wa Bayern, Harry Kane, ambaye hajapata kushinda taji kubwa katika maisha yake ya soka, alikuwa ameketi jukwaani akitarajia kushuhudia timu yake ikitwaa ubingwa. Hata hivyo, bao hilo la dakika za mwisho lilimwacha akiwa na simanzi na mshangao. Kwa upande mwingine, mashabiki wa Leipzig walishangilia kwa nguvu, wakifurahia kuizuia Bayern kusherehekea ubingwa kwenye uwanja wao wa nyumbani. Bayern sasa wanalazimika kusubiri matokeo mengine au mechi yao ijayo ili kuthibitisha ufalme wao katika soka la Ujerumani.
Chanzo cha picha: AP, Reuters