Ulimwengu wa soka na burudani umekutana kwa namna ya kipekee baada ya nyota maarufu wa muziki wa hip hop kutoka Marekani, Snoop Dogg, kutangazwa rasmi kuwa mmoja wa wamiliki na mwekezaji katika klabu ya Swansea City, inayoshiriki ligi daraja la pili nchini Uingereza (Championship).
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa kwenye tovuti ya klabu hiyo mnamo Julai 17, Swansea City imethibitisha ujio wa gwiji huyo wa muziki, hatua ambayo imepokelewa kwa mshangao na hamasa kubwa na mashabiki wa soka duniani kote. Ujio wa Snoop Dogg unafuatia hatua ya kiungo mahiri wa zamani wa Real Madrid na nahodha wa Croatia, Luka Modrić, ambaye naye hivi karibuni alinunua hisa na kuwa mmiliki mwenza wa klabu hiyo.
Taarifa ya klabu ilieleza: "Tunatumai kuwa umaarufu mkubwa wa Snoop Dogg duniani kote na mapenzi yake kwa mchezo wa soka vitasaidia kuitangaza jina la Swansea City kimataifa na kuchangia katika ukuaji wa klabu yetu."
Hatua hii inakuja baada ya awali Snoop Dogg kuibua gumzo kwenye mitandao ya kijamii aliposhiriki katika kutangaza jezi mpya za klabu hiyo kwa msimu wa 2025-2026, kitendo kilichoashiria kuwepo kwa uhusiano wa karibu kati yake na klabu hiyo ya Wales.
Akizungumzia uwekezaji wake, Snoop Dogg alisema, "Mapenzi yangu kwa mchezo wa soka si siri. Hivyo, kupiga hatua yangu ya kwanza kama mmiliki katika klabu ya Swansea City ni jambo la kipekee sana kwangu."
Ili kusherehekea na kuukaribisha ujio wake, picha kubwa ya ukutani (mural) ya sura yake imechorwa na kuzinduliwa katika eneo la jukwaa la magharibi la uwanja wa nyumbani wa Swansea City. Kuungana kwa Snoop Dogg na Luka Modrić kama wamiliki kunaashiria mwanzo wa enzi mpya yenye matumaini kwa klabu hiyo, ikitarajiwa kuvutia wawekezaji zaidi na kuongeza ushindani wake uwanjani.