Katika kile kinachoonekana kuwa pigo kwa ushindani wa kidemokrasia katika soka nchini, Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imetangaza matokeo ya usahili wa wagombea, ambapo jina la rais anayemaliza muda wake, Wallace Karia, limepitishwa likiwa peke yake huku wagombea wengine watano wakienguliwa kwenye kinyang'anyiro hicho.
Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Wakili Kiomoni Kibamba, alisema kati ya wagombea sita waliojitokeza kuwania nafasi ya urais, ni Karia pekee aliyekidhi vigezo vyote vya kikanuni. Alifafanua kuwa wagombea wengine wanne waliondolewa kwa kutokidhi matakwa ya kanuni, huku mmoja wao akiwa hakutokea kabisa kwenye usahili.
"Kwenye nafasi ya urais, mgombea mmoja amekidhi matakwa yote na tumempitisha, ambaye ni Wallace Karia," alisema Wakili Kibamba, kauli inayoacha uchaguzi huo kuwa na mgombea mmoja tu hadi sasa.
Matokeo hayo yana maana kuwa, endapo hali itabaki kama ilivyo, Karia anatarajiwa kuchaguliwa bila kupingwa katika uchaguzi mkuu ujao wa shirikisho hilo.
Wakili Kibamba aliongeza kuwa mchujo huo ulihusu pia nafasi za ujumbe wa kamati ya utendaji, ambapo kati ya wagombea 19 waliofanyiwa usahili, wagombea 10 walipitishwa huku saba wakienguliwa kwa kukosa vigezo.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa mlango bado uko wazi kwa wale walioenguliwa. Alisema wagombea wote ambao majina yao yamekatwa wana haki ya kukata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF endapo wanaona hawakutendewa haki.
"Sisi ni binadamu, inawezekana kuna ambao watahisi wameonewa. Wana nafasi ya kwenda kukata rufaa. Kamati ya Rufaa ikiridhika na hoja zao na kuturudishia majina yao, sisi tutayapokea na kuendelea na mchakato wa uchaguzi," alihitimisha Kibamba, akiacha matumaini ya kuwepo kwa ushindani mikononi mwa Kamati ya Rufaa.
Sasa macho na masikio ya wadau wote wa soka nchini yanaelekezwa kwenye Kamati ya Rufaa, kusubiri kuona kama itaweza kubadili upepo na kurejesha ushindani katika uchaguzi huu muhimu kwa mustakabali wa soka la Tanzania.