Soka la England limepoteza sifa yake ya ‘nyumbani kwa soka’ baada ya kupigwa bao 3-1 na Senegal katika mechi ya kirafiki iliyochezwa huko The City Ground, Nottingham. Kipigo hiki kimekuwa cha kihistoria kwa England, kwani ni mara ya kwanza kwao kufungwa na timu kutoka Afrika.
Mechi hiyo, iliyofanyika Juni 11, ilianza vizuri kwa England, ambapo mshambuliaji wao tegemeo, Harry Kane wa Bayern Munich, aliifungia bao la kuongoza dakika ya 7 tu. Bao hilo lilitokana na shinikizo kali la England katika eneo la hatari la Senegal. Anthony Gordon alipiga shuti kali lililogonga mikono ya kipa na kumfikia Kane, ambaye hakusita kulitia kimiani kwa mguu wa kushoto.
Hata hivyo, furaha ya England haikudumu. Senegal, ilionyesha uthubutu mkubwa na kujibu mashambulizi hayo. Dakika ya 40 ya kipindi cha kwanza, Ismaila Sarr wa Crystal Palace alisawazisha baada ya kupokea pasi murua kutoka kwa Nicolas Jackson wa Chelsea, na kufanya matokeo kuwa 1-1 hadi mapumziko.
Baada ya mapumziko, Senegal iliendeleza kasi. Dakika ya 62, Habib Diarra wa Strasbourg alifunga bao la pili la kugeuza matokeo, akitumia pasi ndefu kutoka nyuma na kuishinda ngome ya England. England ilijaribu kurudi mchezoni na kupata bao kupitia kwa Jude Bellingham wa Real Madrid dakika ya 84, lakini bao hilo lilikataliwa baada ya ukaguzi wa VAR kuonyesha kuwa Levi Colwill wa Chelsea alishika mpira kwa mkono kabla ya bao.
Kwenye dakika za nyongeza, Senegal iliweka msumari wa mwisho kwenye jeneza la England. Katika shambulizi la kushtukiza, Cheikh Sabaly wa Metz alifunga bao la tatu, na kuhakikisha ushindi wa kihistoria kwa timu yake.
Kipigo hiki kimemaliza rekodi ya England ya kutofungwa na timu za Afrika katika mechi 21 zilizopita, ambapo walikuwa wameshinda mechi 15 na kutoa sare 6. Hii pia ni mara ya kwanza kwa England kuruhusu mabao matatu katika mechi moja dhidi ya timu ya Afrika. Kocha wa England, Thomas Tuchel, ambaye alikuwa ameanza na rekodi ya kushinda mechi tatu mfululizo tangu alipoichukua timu hiyo, amepata kipigo chake cha kwanza.
England, ambayo inashika nafasi ya 4 kwenye viwango vya FIFA, ilishuka uwanjani ikiwa na mfumo wa 4-4-2 dhidi ya Senegal (nafasi ya 19 duniani). Walipanga washambuliaji wawili, Kane na Eberechi Eze (Crystal Palace), huku winga wakitumika Anthony Gordon (Newcastle) na Bukayo Saka (Arsenal). Kabla ya mechi hii, England ilikuwa imetoka kucheza mechi ya Kundi K ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Andorra huko Barcelona (ushindi wa 1-0), na walifanya mabadiliko makubwa katika kikosi cha kwanza, wakibadilisha wachezaji 10 kati ya 11, isipokuwa Harry Kane pekee.