Hali ya sintofahamu na matumaini makubwa ilitawala miongoni mwa mashabiki wa FC Barcelona wiki hii. Hii ilitokana na gwiji wao mkuu wa kihistoria, Lionel Messi, kufanya ziara ya ghafla kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Camp Nou, ambao kwa sasa unafanyiwa ukarabati mkubwa.
Mnamo tarehe 10 Novemba, Messi alichapisha picha akiwa ndani ya uwanja huo ulio tupu na kuandika ujumbe uliochoma mioyo ya wengi: "Usiku wa jana nilirudi mahali ambapo ninapamiss (ninapakumbuka) kutoka kwenye kina cha roho yangu. Mahali ambapo nilijisikia furaha isiyo na kikomo... Natumai nitaweza kurudi tena siku moja. Sikuweza kutoa kwaheri yangu nikiwa mchezaji, lakini natumai kwa dhati nitaweza kufanya hivyo siku hiyo."
Ujumbe huu, ulioandikwa kama ungamo la moyoni, ulizua mjadala mkubwa duniani kote, huku mashabiki wakianza kuota ndoto za 'Mfalme' kurejea nyumbani kumalizia maisha yake ya soka.
Hata hivyo, Rais wa klabu hiyo, Joan Laporta, ameingilia kati na kuzima ndoto hizo kwa kauli ya kidiplomasia lakini yenye msimamo mkali. Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kitabu hapo jana (Novemba 13), Laporta alijibu maswali kuhusu ziara hiyo ya Messi. Alisema, "Ziara ya Messi ilikuwa ya hiari yake na inaonyesha roho ya Barcelona. Sikujua kuhusu hilo. Uwanja wa Camp Nou ni nyumba yake. Anaweza kurudi wakati wowote."
Lakini alipoulizwa kuhusu uwezekano wa Messi kurejea kama mchezaji, Laporta alikuwa mkweli na kusema wazi: "Kurejea kwa Messi kama mchezaji si jambo la kweli (unrealistic). Tayari ameshakuwa na wasifu mkuu wa soka na kwa sasa anacheza kwenye jukwaa tofauti." Kauli hii inathibitishwa na ukweli kwamba Messi bado ana mkataba mrefu na klabu yake ya Inter Miami nchini Marekani, unaotarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Licha ya kufunga mlango wa yeye kuvaa tena jezi ya Barcelona, Laporta alitangaza habari njema kwa mashabiki. Alithibitisha kuwa klabu ina mpango thabiti wa kumjengea Messi sanamu lake la heshima nje ya uwanja wa Camp Nou, pembeni ya magwiji wengine wakubwa wa klabu hiyo.
"Nimekuwa nikifikiria na wenzangu kwenye bodi kwamba tunatakiwa kumpa Messi heshima zaidi," alisema Laporta. "Messi anastahili sanamu lake pale Camp Nou, kama walivyo Johan Cruyff na László Kubala. Yeye ni mchezaji aliyetuathiri sote. Tutaandaa mradi wa sanamu wenye ubora wa hali ya juu na kuupeleka kwa familia yake ili kupata idhini. Bila shaka mashabiki watapenda kuona sanamu la Messi likisimama pale."
Rais huyo pia aligusia tena tukio la mwaka 2021 lililomlazimu Messi kuondoka klabuni hapo kutokana na matatizo ya kifedha. Laporta alisisitiza kuwa ingawa hakupenda mambo yawe vile, "hana majuto" kwa sababu klabu ya Barcelona ni kubwa kuliko mchezaji yeyote.
Kwa kauli hizi, ni wazi kwamba uhusiano wa Messi na Barcelona kama mchezaji umefikia mwisho, lakini heshima yake kama gwiji wa klabu itadumishwa kupitia sanamu hilo la kihistoria na labda mechi ya kumuaga.