Klabu ya soka ya Chelsea inakabiliwa na uwezekano wa kutozwa faini na Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) kwa kukiuka sheria zake za Uendeshaji Bora wa Kifedha (FFP). Taarifa kutoka gazeti la Uingereza la The Times zinasema kuwa UEFA inaamini Chelsea ilikiuka sheria hizo kwa kuuza timu yake ya wanawake na hoteli kwa kampuni zinazohusiana nayo, hatua ambayo UEFA haioni kama mikataba huru na haitaki itumike kufidia hasara za uendeshaji wa klabu. Hali hii inaweza kuifanya Chelsea kuvuka kiwango cha juu cha hasara kinachoruhusiwa na UEFA.
Hivi karibuni, Chelsea ilitoa ripoti ya kifedha iliyoonyesha faida ya pauni milioni 180. Hata hivyo, sehemu iliyoibua wasiwasi ni "faida kutokana na mauzo kwa kampuni zinazohusiana" iliyofikia pauni milioni 198.7. Hii inahusu uuzaji wa timu ya wanawake ya Chelsea Women kwa kampuni ya BlueCo, ambayo ni kampuni mama iliyoanzishwa na mmiliki wa klabu, Todd Boehly, na kampuni ya uwekezaji ya Clearlake Capital kwa ajili ya kuinunua Chelsea.
Msemaji wa Chelsea alielezea uuzaji wa timu ya wanawake kwa BlueCo kama "uhamishaji wa kimkakati" akisema kuwa hatua hiyo itawezesha timu ya wanawake kuwa na uongozi bora katika masuala ya uendeshaji na biashara, hivyo kuwezesha ukuaji na mafanikio zaidi. Licha ya maelezo hayo, kuna mtazamo unaoenea kuwa Chelsea ilitumia mbinu hii ya kuuza timu kwa kampuni inayohusiana nayo ili kuepuka kuonekana na hasara kwenye vitabu vyake vya hesabu.
The Times liliripoti kuwa uuzaji wa timu ya wanawake uliwezesha Chelsea kukwepa kuvunja sheria za mapato na uendelevu za Ligi Kuu ya Uingereza (PSR). Chelsea imekuwa ikifanya uwekezaji mkubwa katika usajili wa wachezaji kila msimu, na gharama ya uhamisho imezidi pauni bilioni 1. Gazeti hilo liliongeza kuwa ingawa Ligi Kuu inaruhusu mapato yanayotokana na mikataba na kampuni tanzu au zinazohusiana (APT), UEFA hairuhusu hilo. Naye gazeti la Daily Mail lilikazia kuwa ingawa Ligi Kuu inaruhusu APT, mikataba hiyo inapaswa kufanywa kwa bei halisi ya soko, na kudai kuwa faida ambayo Chelsea imetangaza ni matokeo ya kutumia mianya ya PSR kupitia APT.
Kama ilivyotarajiwa, hatua ya UEFA inaonekana kuiweka Chelsea katika hali ngumu. The Times linaripoti kuwa Chelsea inajadiliana na UEFA kuhusu suluhu inayoweza kujumuisha faini na pia onyo la kutoshiriki kwenye mashindano ya klabu za Ulaya iwapo itarudia kosa. Inawezekana pia Chelsea ikakubali mpango wa UEFA wa kudhibiti matumizi kwa misimu mitatu ijayo. UEFA inatarajiwa kutoa uamuzi wake kuhusu suala hili katikati ya mwezi ujao.
Adhabu kutoka UEFA inaweza isiwe mwisho wa matatizo kwa Chelsea. Bado haijajulikana kama Ligi Kuu ya Uingereza itafanya uchunguzi wake kuhusu suala hili. Hata hivyo, kwa kuzingatia uchunguzi mkubwa ambao Manchester City inafanyiwa kwa madai ya kukiuka sheria za PSR na uwezekano wa kuadhibiwa, ni vigumu kwa Chelsea kupuuza hali hii.
Chelsea, pamoja na Manchester City, ni miongoni mwa timu zilizokua kwa kasi kubwa katika karne ya 21. Mwanzoni mwa miaka ya 2000, baada ya bilionea wa Urusi Roman Abramovich kuinunua klabu, alifanya uwekezaji mkubwa ambao ulipelekea timu kufanya vizuri sana na kushinda mataji mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Ligi Kuu ya Uingereza na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hata hivyo, baada ya vikwazo vya kiuchumi vilivyotokana na vita kati ya Urusi na Ukraine, Abramovich alipokonywa umiliki wa klabu, na kuanza kipindi cha sintofahamu. Baada ya kubadilishwa kwa mmiliki, kuna wasiwasi unaoongezeka kuwa Chelsea inaingia kwenye kipindi kigumu, na adhabu hii kutoka UEFA inaweza kuharakisha zaidi hali hiyo.