Hasira za Rüdiger Fainali zaweza Kumponza Vibaya, Adhabu Kali Yamkabili

sports | Mon Apr 28 2025


Hasira za Rüdiger Fainali zaweza Kumponza Vibaya, Adhabu Kali Yamkabili

Beki kisiki wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ujerumani, Antonio Rüdiger, anakabiliwa na uwezekano wa kufungiwa kwa muda mrefu kufuatia vituko alivyoonesha wakati wa fainali ya Kombe la Mfalme (Copa del Rey) dhidi ya Barcelona, ambapo timu yake ilipoteza kwa mabao 3-2 baada ya muda wa ziada.


Vyombo vya habari nchini Hispania, kama vile gazeti la Marca, vinaripoti kuwa mwamuzi wa mchezo huo, Ricardo de Burgos Bengoetxea, alitoa kadi nyekundu kwa wachezaji watatu wa Real Madrid katika dakika za lala salama za mchezo huo uliofanyika Jumapili (Aprili 27, 2025) mjini Seville. Hali hiyo ilichangiwa na Real Madrid kupoteza mchezo huo muhimu baada ya kuongoza 2-1 hadi dakika za mwisho za kipindi cha pili.



Tatizo kubwa zaidi, hata hivyo, linaweza kuwa adhabu inayomkabili Rüdiger kutokana na namna alivyolipuka kwa hasira. Mwamuzi De Burgos alipopuliza kipyenga kuashiria faulo iliyofanywa na Kylian Mbappe, Rüdiger, ambaye alikuwa kwenye benchi la wachezaji wa akiba, aliripotiwa kurusha kitu (bila kufafanuliwa ni kitu gani) na kujaribu kuingia uwanjani kwa hasira kabla ya kuzuiwa na wachezaji wenzake na maafisa wa timu. Hata baada ya kuzuiwa, Rüdiger alionekana akimtolea mwamuzi maneno makali yaliyoonekana kama matusi, kitendo kilichopelekea kuoneshwa kadi nyekundu moja kwa moja na kuamriwa kuondoka kwenye benchi.


Gazeti la Marca linaeleza kuwa ingawa maafisa wa Real Madrid walifanikiwa kumzuia Rüdiger na kuepusha shari kubwa zaidi, bado kuna uwezekano mkubwa akakumbana na adhabu kali kutoka kwa shirikisho la soka la Hispania.


Kitendo hiki hakikuishia kwa Rüdiger pekee. Beki mwingine, Lucas Vazquez, naye alioneshwa kadi nyekundu kwa kumkabili mwamuzi kwa maneno makali. Ripoti ya mwamuzi pia inaeleza kuwa kiungo Jude Bellingham alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumkimbilia mwamuzi kwa mtindo wa uchokozi au ukali.


Ukubwa wa adhabu anayoweza kupata Rüdiger unatia hofu. Kituo cha habari cha BBC kimeangazia kanuni za shirikisho la soka Hispania. Kifungu cha 101 kinachohusu "vurugu ndogo" dhidi ya mwamuzi kinaweza kusababisha adhabu ya kufungiwa kati ya mechi 4 hadi 12. Hata hivyo, ikiwa kitendo chake kitatafsiriwa kuwa kibaya zaidi na kuingia kwenye Kifungu cha 104 kinachohusu "uchokozi/ushambulizi" dhidi ya mwamuzi, adhabu inaweza kuwa kali zaidi: kifungo cha miezi mitatu hadi sita ikiwa kitendo ni kimoja na hakikusababisha madhara. Adhabu hiyo inaweza kuongezwa hadi kufikia miezi sita au hata mwaka mzima ikiwa kitendo kitaonekana kuleta "hatari kubwa" hata kama mwamuzi hakuhitaji matibabu.


Inafaa kukumbuka kuwa Real Madrid waliingia kwenye mchezo huu wakiwa tayari wamechemsha hali ya hewa kuhusu uteuzi wa mwamuzi De Burgos. Klabu hiyo ilisusa kuhudhuria mkutano na waandishi wa habari kabla ya mchezo, mazoezi rasmi, na upigaji picha rasmi kama njia ya kupinga uteuzi huo. Walidai kuwa De Burgos ana historia ya kuwabana na walitengeneza video kumkosoa. Kitendo hiki kilizua mjadala mkubwa na huenda kilichangia hali ya taharuki iliyojitokeza uwanjani.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.