Azam Yamfunga Fei Toto kwa Mshahara Mnono Zaidi Ligi Kuu

sports | Wed Aug 27 2025


Azam Yamfunga Fei Toto kwa Mshahara Mnono Zaidi Ligi Kuu

Baada ya miezi kadhaa ya minong'ono na tetesi zilizotikisa ulimwengu wa soka nchini, Klabu ya Azam FC imefunga rasmi mjadala kuhusu mustakabali wa kiungo wake fundi, Feisal Salum 'Fei Toto'. Uongozi wa klabu hiyo umeweka nukta kwa kutangaza kuwa mchezaji huyo ameongeza mkataba wa mwaka mmoja, na kumuweka rasmi kama mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kuliko wote wanaokipiga katika Ligi Kuu ya Tanzania.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat', alivunja ukimya na kufafanua sakata zima lililomzingira nyota huyo. Popat alisisitiza kuwa, kinyume na taarifa zilizosambaa mitandaoni, hakuna klabu yoyote ya hapa nchini, akiwemo vigogo Simba na Yanga, iliyowahi kuwasilisha ofa rasmi mezani kwa ajili ya kumsajili Fei Toto.


"Sakata la Fei Toto halikuwa gumu kama lilivyokuwa likiripotiwa. Ukweli ni kwamba, mchezaji mwenyewe hakuwahi kutufuata hata siku moja kutuambia anataka kuondoka," alisema Popat. Aliongeza kuwa, ingawa kulikuwa na timu moja kutoka nje ya nchi iliyoonyesha nia, ilishindwa kufikia dau ambalo Azam FC waliliweka, na hivyo mazungumzo hayakufika mbali.


Alifafanua kuwa kuchelewa kusaini mkataba mpya kulisababishwa na taratibu za kawaida za majadiliano, ambapo pande zote mbili zinapaswa kuridhia vipengele vilivyomo kabla ya kuweka saini. "Mkataba ni makubaliano. Ni lazima pande mbili ziridhie. Kama kuna vipengele hamjakubaliana, hauwezi kusainiwa. Hilo ndilo lililokuwa linaendelea," alieleza.


Hatimaye, Popat alitangaza habari njema kwa mashabiki wa Azam FC, akisema: "Leo naweza kusema rasmi kuwa suala hili limekwisha. Ameongeza mkataba wa mwaka mmoja ambao utamfanya abaki hapa Chamazi hadi mwaka 2027."


Alimalizia kwa kusema mkataba huo mpya una maboresho makubwa ambayo yanamfanya Fei Toto kuwa mchezaji anayelipwa fedha nyingi zaidi, akiwapita wachezaji wote wa ndani na wa kigeni wanaocheza soka Tanzania. Hii inazima rasmi ndoto za klabu za Simba, Yanga, na hata Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini zilizokuwa zikihusishwa na harakati za kuiwania saini yake.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.