Watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, wamepewa jukumu la kuhakikisha wanasimamia na kuratibu kwa umakini taarifa za utekelezaji wa miradi ya Serikali ya Awamu ya Sita na kuzifikisha kwa wananchi. Lengo ni kuwawezesha wananchi kuelewa maendeleo yanayotekelezwa katika maeneo yao na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.
Wito huo ulitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, wakati wa kufungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi cha ofisi hiyo, kilichofanyika Machi 14, 2025, katika Ukumbi wa Ngome, jijini Dodoma.
Waziri Lukuvi alisisitiza kuwa watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha uwajibikaji katika kazi za serikali na usimamizi wa shughuli zake. Hii ni pamoja na kuratibu na kuwasilisha taarifa za maendeleo kwa wananchi kwa usahihi na kwa wakati.
"Tunalo jukumu la kuwaeleza wananchi kazi zilizotekelezwa na Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha uongozi. Hili ni jukumu letu la msingi kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu maendeleo yanayofanyika," alisema Waziri Lukuvi.
Aliongeza kuwa ili uratibu wa taarifa za serikali uwe na mafanikio, ni muhimu kuhakikisha majukumu ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu yanasimamiwa vyema. Hii itawezesha ofisi hiyo kusimamia ipasavyo taasisi na idara zilizo chini yake, na kuhakikisha ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha, Waziri Lukuvi alieleza kuwa Waziri Mkuu ana imani kubwa na watendaji wa ofisi yake, na hivyo aliwataka kuendelea kuratibu shughuli zote za serikali kwa ufanisi.
"Nikupongeze Katibu Mkuu, Dk. Yonazi, kwa usimamizi mzuri pamoja na timu yako ya menejimenti. Endeleeni kushirikiana katika kutekeleza majukumu yenu. Pia nawapongeza Wakuu wa Idara na Vitengo kwa kazi nzuri mnayofanya," alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk. Jim Yonazi, alimshukuru Waziri wa Nchi pamoja na Naibu Waziri kwa miongozo mizuri wanayotoa, akisisitiza kuwa hiyo imechangia ufanisi wa utendaji kazi wa watumishi wa ofisi hiyo.
"Viongozi wetu wakuu wanafahamu kazi kubwa tunayoifanya. Kupitia nyie, tunawaomba mfikishe salamu zetu za shukrani kwao," alisema Dk. Yonazi.
Naye Msaidizi wa Katibu wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) Mkoa wa Dodoma, Maisha Mbilla, aliipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuhakikisha kuwa watumishi wake wanafanya kazi katika mazingira mazuri na wanapata stahiki zao ipasavyo.
"Hii inatufariji na kututia moyo. Sisi kama Chama cha Wafanyakazi tunao wajibu wa kuzungumza na watumishi ili waendelee kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya Utumishi wa Umma," alisema Mbilla.
Kikao hicho kimeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, sambamba na kuwashirikisha wananchi katika kufahamu hatua zinazopigwa na Serikali ya Awamu ya Sita.