Akitumia lugha ya picha yenye ujumbe mzito, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amewapuuza watu wachache wanaotumia mitandao ya kijamii kueneza chuki na uchochezi, akiwafananisha na maharage machache yanayoelea juu wakati wa kupika ambayo kamwe hayaivi. Wasira alitoa kauli hiyo yenye kuchekesha na kuchoma leo, Oktoba 9, 2025, katika mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika katika mji wake wa nyumbani wa Bunda, Mkoa wa Mara, kumuunga mkono mgombea urais wa chama hicho, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Mwanasiasa huyo mkongwe alisema kuwa amani na utulivu wa Tanzania haviwezi kutikiswa na kikundi kidogo cha watu wasioridhika ambao wamechagua mitandao ya kijamii kama uwanja wao wa kueneza maneno yasiyofaa. Alisema Watanzania walio wengi wanajua thamani ya amani na wanatambua kazi kubwa inayofanywa na serikali, hivyo hawatasikiliza "chokochoko" hizo.
"Kuna watu hawaridhiki na lolote. Hata mpike maharage vizuri namna gani, lazima yapatikane yale machache yanayoelea juu; hayo hayaivi na ndiyo yanayosumbua. Msibabaishwe na hawa, wako wachache sana," alisema Wasira, huku akimwambia Dk. Samia asiyape uzito maneno yao. "Wako wengi watakaokukumbuka kwa wema na nia njema, na kama mnavyomuunga mkono hapa Bunda, ndivyo anavyoungwa mkono kote nchini."
Katika kumwombea kura Dk. Samia, Wasira alisisitiza kuwa CCM imewaletea wananchi mgombea ambaye si mwanafunzi wa urais, bali ni kiongozi mzoefu aliyethibitisha uwezo wake. Alimlinganisha na dereva mwenye leseni anayekabidhiwa gari jipya, tofauti na mgombea "lena" (mwenye kibali cha kujifunza udereva) ambaye hawezi kuaminiwa.
Alimpongeza Rais Samia kwa kuliongoza taifa kwa ujasiri na utulivu katika vipindi vigumu, vikiwemo janga la UVIKO-19, msiba wa aliyekuwa Rais, Hayati Dk. John Magufuli, na misukosuko ya kiuchumi duniani. Alisema uwezo wake wa kuvusha nchi salama katika nyakati hizo ni uthibitisho tosha kwamba anastahili kuendelea kuongoza.