Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Bwana Stephen Wasira, amepokelewa kwa shangwe na nderemo alipowasili katika Mkoa wa Shinyanga. Mapokezi hayo ya aina yake yalifanyika leo, tarehe 26 Machi, 2025, wakati alipowasili mkoani humo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za chama.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Bwana Wasira aliwashukuru kwa dhati wanachama wote wa CCM mkoani Shinyanga kwa mapenzi makubwa waliyomwonyesha. Alieleza kuwa ziara yake hiyo ina lengo kuu la kuimarisha chama na kuandaa mikakati ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
"Nawashukuru sana wana CCM Shinyanga kwa mapokezi mazuri. Safari yangu hii shabaha yake kubwa ni kuimarisha chama. Chama chetu ni chama kikubwa wala siyo cha msimu kama vingine, baada ya uchaguzi vinakufa. Na shughuli yetu sisi CCM ni kubadilisha maisha ya watu na kushughulikia matatizo yao, ndiyo shabaha yetu ya msingi," alisisitiza Bwana Wasira.
Aidha, alieleza kuwa chama hicho kimejiandaa kikamilifu kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu. Aliongeza kuwa yajayo yanafurahisha na kuwataka wanachama wa CCM kuendelea kuwa imara na kuunga mkono juhudi za chama katika kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Bwana Mabala Mlolwa, alimkaribisha Bwana Wasira mkoani humo na kueleza kuwa wanafurahi sana kwa ujio wake. Aliahidi kuwa wanachama wa CCM mkoani Shinyanga watahakikisha kuwa wanafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha chama kinashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao.
Ziara ya Bwana Stephen Wasira ilianza leo, tarehe 26 Machi, na itahitimishwa tarehe 28 Machi, 2025. Ziara hii inatarajiwa kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya chama na kuandaa mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto za wananchi.