Wasira Amjibu Zitto Kabwe: CCM Haiogopi Mazungumzo na CHADEMA, Waeleze Wanachotaka

politics | Mon Mar 31 2025


Wasira Amjibu Zitto Kabwe: CCM Haiogopi Mazungumzo na CHADEMA, Waeleze Wanachotaka

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amejibu madai ya kiongozi mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, akisisitiza kuwa CCM iko tayari kwa mazungumzo na CHADEMA, lakini chama hicho hakiko tayari kueleza wazi mabadiliko wanayoyataka.



Wasira aliyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu, ambapo maelfu ya wananchi walihudhuria. Alitumia fursa hiyo kujibu kauli ya Zitto Kabwe, aliyedai kutoka Lindi kuwa Wasira anajua historia, na hivyo anapaswa kuzungumza na CHADEMA badala ya kubishana nao.




"Mimi niliwaambia tuzungumze, lakini Tundu Lissu alisema tutawapotezea muda. Sasa, mtu ambaye ana muda wake na hataki upoteze, kwanini umlazimishe? Kwa hiyo, tunawaambia, ikiwa wana jambo linalozungumzika na linawezekana, waje tuzungumze," alieleza Wasira.



Aliongeza kuwa, CHADEMA hawako tayari kuzungumza, na wanadai mabadiliko ambayo yeye (Wasira) hayajui na hawajayataja. "Leo nataka niwaambie, mtuambie mnataka nini hasa, maana wanazungumzia 'no reform, no reform', 'reform' gani? Tumeshafanya 'reform' nyingi," alisema.


Wasira alibainisha kuwa, CHADEMA wanapaswa kuwaambia Watanzania mabadiliko wanayoyataka, kwani wanachama wao wameanza kuwahama. "Wanachama wao wameanza kuwageuka, na wanataka kugombea udiwani. Hata kama hawataupata, tunawapa uhuru wa kuongea," alisema.


Akizungumzia madai ya Zitto Kabwe kuwa CCM imekataa kukaa na CHADEMA, Wasira alisema hiyo si kweli, akieleza kuwa CCM ni mwanachama wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), ambacho kinaongozwa na Tundu Lissu. "Akiitisha kikao, tutaenda. Sisi ni watu wa amani, hatutaki shari," alisisitiza.


Wasira alimalizia kwa kuwataka CHADEMA kujitokeza hadharani na kueleza wanachotaka, na ikiwa wanashindwa kuiambia CCM, basi waiambie Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.