Katika hatua ya kimkakati ya kukabiliana na ongezeko la habari za uongo na upotoshaji unaolenga taasisi na umma, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kuanzishwa kwa mfumo wa kisasa wa kutumia 'QR Code' ili kuwapa wananchi uwezo wa kuthibitisha uhalisi wa taarifa zake rasmi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Ndugu Amos Makalla, alisema hatua hii inalenga kupambana moja kwa moja na watu wenye nia ovu wanaotumia mitandao ya kijamii kuchafua taswira ya chama na kuzua taharuki nchini.
Mfumo huu mpya unafanya kazi kwa urahisi kupitia simu janja (smartphone). Mwananchi anapokutana na taarifa yoyote inayodaiwa kutoka CCM, anachotakiwa kufanya ni kuchukua simu yake na kufanya 'scan' kwenye alama ya QR Code iliyoambatanishwa. Iwapo taarifa hiyo ni ya kweli, mfumo utampeleka moja kwa moja kwenye chapisho hilo rasmi lililopo kwenye tovuti au kurasa rasmi za mitandao ya kijamii za CCM. Kinyume chake, iwapo taarifa ni ya kupikwa, msomaji akijaribu kutumia QR Code hiyo, hatapata matokeo yoyote, au ataelekezwa kwenye taarifa rasmi inayokanusha uzushi huo.
"Kwa mfano, taarifa ya uzushi iliyosambazwa hivi karibuni tarehe 20 Julai 2025 ilizua sintofahamu. Hata hivyo, mtu yeyote aliyejaribu kuhakiki kwa kutumia QR Code yetu alielekezwa kwenye taarifa sahihi yenye kichwa 'CCM YATOA RAMBIRAMBI KWA AJALI YA GARI – IWAMBI, MBEYA', jambo lililothibitisha mara moja kuwa ile ya awali ilikuwa ni ya uongo," alifafanua Makalla.
Chama Cha Mapinduzi kinatoa wito kwa Watanzania wote na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuwa makini na kutumia teknolojia hii rahisi ili kujilinda dhidi ya upotoshaji. Ndugu Makalla alisisitiza kuwa huu ndio utaratibu rasmi sasa, na ni njia ya uhakika ya kupata habari sahihi kutoka chamani, hatua itakayosaidia kulinda utulivu na mshikamano wa kitaifa.