Mji mkuu wa Uturuki, Ankara, umeshuhudia wimbi kubwa la hasira za wananchi baada ya takriban watu 50,000 kumiminika mitaani kupinga kile walichokiita ukandamizaji wa kisiasa unaofanywa na serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan dhidi ya chama kikuu cha upinzani nchini humo. Maandamano haya makubwa yamechochewa na kesi mahakamani inayoweza kukivuruga kabisa chama cha Republican People's Party (CHP).
Kiini cha mzozo huu ni uamuzi wa mahakama unaotarajiwa kutolewa tarehe 15, ambao utahusu uhalali wa matokeo ya uchaguzi wa ndani wa chama cha CHP uliofanyika mwaka 2023. Iwapo mahakama itaamua kuwa uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu, kama inavyodaiwa, na kubatilisha matokeo yake, basi uongozi mzima wa sasa wa chama hicho, akiwemo Mwenyekiti wake Özgür Özel, utapoteza mamlaka yake mara moja. Kitendo hiki kinatafsiriwa na upinzani kama jaribio la serikali la kutumia mahakama kuwaondoa wapinzani wake kisiasa.
Akihutubia umati uliofurika huku wakipeperusha bendera za Uturuki na za chama cha CHP, Kiongozi wa upinzani Özgür Özel, alitangaza kwa ujasiri kwamba wamekusanyika kupinga "mapinduzi ya kimahakama" yaliyoratibiwa dhidi yao. Alisisitiza kuwa kesi hiyo ni njama za kisiasa na kuapa kwamba hawatakubali kushindwa kimyakimya.
"Serikali hii haiitaki demokrasia, kwa sababu wanajua wazi kuwa demokrasia ikisimama, hawawezi kushinda uchaguzi," alisema Özel, huku akishangiliwa na maelfu ya wafuasi. Aliendelea kusema, "Pia hawaitaki haki, kwa sababu wanajua haki ikitendeka, hawawezi kuficha uhalifu wao." Alionya kuwa serikali ya Uturuki sasa inakabiliwa na madhara makubwa ya kuacha njia ya kidemokrasia na kuchagua kutawala kwa ukandamizaji, ambapo yeyote anayeonekana kuwa tishio kwao anageuzwa kuwa shabaha.
Hali ya wasiwasi wa kisiasa nchini Uturuki imekuwa ikiongezeka tangu mwezi Machi, kufuatia kutiwa jela kwa Meya maarufu wa Jiji la Istanbul, Ekrem İmamoğlu, ambaye anatokea chama cha CHP na alionekana kama mshindani mkuu wa urais. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, zaidi ya watu 500, wakiwemo mameya 17 wa chama cha CHP, wamekamatwa na kuwekwa kizuizini chini ya mwavuli wa uchunguzi wa vitendo vya rushwa, hatua ambayo upinzani unaiona kama kampeni ya kuwaangamiza.