Akiwa katika mkutano wa kampeni wilayani Liwale, mkoani Lindi, Mgombea Mwenza wa Urais kupitia CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amefunguka kuhusu mojawapo ya nyakati muhimu zilizomjenga kisiasa, akisimulia wosia mzito aliopewa na Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Rashidi Mfaume Kawawa, siku chache kabla ya kifo chake.
Dk. Nchimbi aliwapeleka wananchi katika safari ya hisia alipokumbuka tukio la Desemba 2009, alipomtembelea Mzee Kawawa hospitalini alipokuwa mahututi. Alieleza kuwa baada ya salamu za awali, alishangaa kupigiwa simu na kuitwa tena na kiongozi huyo. “Nilipofika tulikuwa wachache sana, mimi, watoto wake Victor na Zainab, pamoja na mlinzi. Kwa sauti ya unyonge lakini yenye msimamo, aliniambia wazi kuwa safari yake imefika mwisho. Kisha akanipa agizo zito, akisisitiza nihakikishe Chama Cha Mapinduzi kinabaki kuwa chama cha watu, kimbilio la wanyonge na mtetezi wa wenye shida. Wiki moja haikuisha, mzee wetu alitutoka,” alisimulia Dk. Nchimbi.
Chanzo cha ukaribu huu wa kipekee, alieleza, kilitokana na ushauri wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Dk. Nchimbi alikumbusha kuwa, mara tu alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mwalimu Nyerere alimwita na kumwelekeza. "Nyerere aliniambia, 'Kama unataka kuujua uzalendo wa kweli, nenda ukakae na Rashidi Kawawa, yeye atakufunza'," alisema Nchimbi, akibainisha kuwa wakati huo Kawawa alikuwa Kamanda Mkuu wa UVCCM.
Dk. Nchimbi amesisitiza kuwa falsafa na wosia huo wa Mzee Kawawa ni deni analobeba na ataendelea kuuenzi. Ameahidi kuwa, kupitia Ilani ya CCM, serikali ijayo itahakikisha inajenga mifumo imara ya hifadhi ya jamii na kisiasa inayomlinda na kumuinua kila Mtanzania, hasa wale walio wanyonge, kama urithi endelevu wa waasisi wa taifa.