Hali ya hewa ya kisiasa katika Jimbo la Kigoma Kaskazini imechamka upya baada ya Mbunge wa jimbo hilo kupitia tiketi ya chama cha ACT Wazalendo, Mhe. Kiza Mayeye, kuvunja ukimya na kuweka bayana msimamo wake kuhusu utumishi wa umma. Katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika Novemba 30, 2025, katika Uwanja wa Mwandiga, Mayeye amewaambia wapiga kura wake kuwa yeye hakuenda Dodoma kutafuta ukwasi wala maisha mazuri binafsi, bali ameenda kama 'mtumwa' wa wananchi ili kutatua kero sugu zinazozikabili kata zote 16 za jimbo hilo.
Nadhiri ya Vifaa vya Kujifungulia Akizungumza kwa hisia mbele ya umati uliofurika uwanjani hapo kumshukuru kwa ushindi, Mayeye aliweka wazi kuwa anajua uchungu wa kina mama vijijini. Aliahidi kuwa mara baada ya Bunge la Bajeti la Februari 2026, atahakikisha anatekeleza ahadi yake ya "kibabe" ya kuwapatia wajawazito vifaa muhimu vya kujifungulia (delivery kits).
"Ndugu zangu, sitaki ubunge ili nijenge majumba au niendeshe magari ya kifahari wakati mama zetu wanateseka zahanati. Nataka ubunge ubadili maisha yenu. Ahadi yangu iko palepale; beseni, mipira, na wembe vitapatikana ili mama ajifungue kwa staha na usalama. Huu ni mkakati wa kupunguza vifo vya mama na mtoto," alisisitiza Mayeye huku akishangiliwa.
Elimu na Mfuko wa Jimbo Kuhusu sekta ya elimu ambayo ni uti wa mgongo wa maendeleo, Mbunge huyo alibainisha kuwa Fedha za Mfuko wa Jimbo hazitaliwa na "wajanja". Badala yake, zitaelekezwa kuboresha miundombinu ya shule, hususan utengenezaji wa madawati ili kumaliza aibu ya wanafunzi kukaa chini. Aidha, aligusia mpango wa chakula shuleni kama nyenzo ya kuwapunguzia mzigo wazazi na kuongeza ufaulu.
Kilio cha Mikopo na "Samaki Nyamnyam" Mkutano huo ulibadilika na kuwa jukwaa la kuchambua kero za kitaifa pale Mwenyekiti Mstaafu wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Kigoma, Mzee Sendwe Ibrahim, alipopanda jukwaani na kuwasilisha kilio cha wazazi kuhusu Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Mzee Sendwe alilalamikia utaratibu wa sasa unaowaacha watoto wa masikini wakitaabika huku wazazi wakilazimika kuuza mifugo na mali zao. "Mheshimiwa Mbunge, kase-mee hili bungeni kwa nguvu zote. Tunataka serikali iweke sheria, kima cha chini cha mkopo kiwe asilimia 50 kwa kila mwanafunzi. Haiwezekani wazazi huku vijijini wanauza ng'ombe kusomesha watoto halafu mikopo inatoka kwa upendeleo au kiduchu," alifoka Mzee Sendwe.
Suala la Uvuvi katika Ziwa Tanganyika nalo lilichukua nafasi kubwa. Imebainika kuwa kuna mkanganyiko mkubwa wa sheria za uvuvi kati ya nchi zinazozunguka ziwa hilo. Mzee Sendwe alieleza kuwa wakati Tanzania inazuia uvuvi wa samaki wadogo aina ya "Nyamnyam", wenzetu wa Burundi wanavua bila shida, jambo linaloleta ushindani usiokuwa wa haki na kuchochea uvuvi haramu. Alitaka kuwepo kwa uwiano wa sheria (harmonization of laws) ili kulinda rasilimali za ziwa hilo kwa faida ya wote.
Vilevile, kero ya wanafunzi wa vyuo kukosa barua za utambulisho kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo (Field Attachment) ilijadiliwa, huku serikali ikitakiwa kutoa mwongozo thabiti kwa vyuo ili vijana wasihangaike mitaani kutafuta nafasi hizo kienyeji.
Mbunge Sio ATM Katika kuhitimisha, Meneja wa Kampeni wa Mbunge huyo, Bw. Shaban Mambo, alitoa "shule" kwa wananchi kuhusu dhana ya utegemezi. Aliwaasa vijana na wananchi kuacha kumgeuza mbunge kuwa mashine ya kutolea fedha (ATM) kwa shida binafsi, kwani mshahara wake hauwezi kutosheleza kila mtu.
"Tusilete shida za 'niongezee elfu kumi', leteni mawazo ya miradi. Vijana anzisheni akademi za mpira, limeni nyanya mpeleke Congo, vueni samaki kisasa. Mbunge kazi yake ni kuwapambania sera nzuri na mazingira rafiki ya biashara, siyo kugawa pesa mkononi," alisisitiza Mambo.
Mkutano huu umefungua ukurasa mpya kwa Kigoma Kaskazini, huku wananchi wakiwa na matumaini makubwa ya kuona ahadi hizo zikitekelezwa na kero za mpakani zikipatiwa ufumbuzi wa kidiplomasia.