Rais Samia Suluhu Hassan amewaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni, akiwemo aliyekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Amos Makalla, ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha. Katika hafla hiyo ya kuapishwa, Rais Samia alimpa Makalla maagizo mazito yanayohusu maendeleo ya mkoa huo maarufu kwa utalii na biashara. Makalla anachukua nafasi ya Kenan Kihongosi, aliyedumu katika nafasi hiyo kwa takribani miezi miwili.
Rais Samia alimshukuru Makalla kwa kazi kubwa aliyoifanya katika nafasi yake ya awali ya uenezi wa CCM, akisema amejenga umoja ndani ya chama. Alisisitiza kuwa uamuzi wa kumrudisha serikalini unalenga kumtumia ujuzi wake mkubwa na uzoefu wa utumishi wa umma. “Wewe si mgeni. Umeshakuwa mkuu wa mkoa katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Dar es Salaam na Arusha. Nina imani utaliweza vizuri jukumu hili,” alisema Rais.
Katika maagizo yake, Rais alimwelekeza Makalla kusimamia vyema maendeleo ya Mkoa wa Arusha, akitambua umuhimu wake kiuchumi na kama kitovu cha utalii na diplomasia nchini. Rais Samia alitaja mipango kabambe ya serikali, ikiwemo ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa mazingira kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027. Alimwagiza Makalla kuhakikisha kazi hiyo inakamilika vyema na kuhamasisha wananchi kutumia fursa hiyo kujipatia kipato na kukuza uchumi wa mkoa.
Maagizo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma
Kwa upande wa Katibu Tawala mpya wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Khatib Kazungu, Rais Samia alimwagiza kwenda kusimamia miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa katika makao makuu ya nchi. Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria, ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, barabara kubwa za mzunguko, pamoja na ujenzi wa mji wa serikali.
Rais alisisitiza kuwa Dodoma inakua kwa kasi kubwa, na idadi ya watu inaongezeka kwa kasi zaidi. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, kasi ya ongezeko la watu Dodoma imefikia asilimia 3.9, ikilinganishwa na asilimia 1.2 ya awali. Ongezeko hilo linahitaji uongozi imara kusimamia maendeleo na mahitaji ya huduma za kijamii.
Matarajio ya Watanzania kwa Utumishi wa Umma
Akizungumzia Tume ya Utumishi wa Umma, Rais Samia alieleza kuwa Watanzania wana matarajio makubwa manne kutoka kwa utumishi huo, kulingana na Dira ya Taifa ya 2050. Kwanza, wanataka utumishi unaozingatia uadilifu, sifa na uwezo katika kuajiri na kupandisha vyeo. Pili, wanataka utumishi wa umma unaoendana na maendeleo ya kiteknolojia. Tatu, wanataka utumishi wa umma wenye uwazi na uadilifu, unaopambana na rushwa. Na la nne, wanataka utumishi wa umma unaotambua na kuunga mkono maendeleo ya sekta binafsi. Rais Samia alitangaza kuwa bajeti ya utumishi wa umma itaongezwa ili kuwezesha utekelezaji wa matarajio haya.