Hali ya wasiwasi wa kisiasa imetanda mkoani Pwani baada ya Jeshi la Polisi kutangaza kuwashikilia watu 10, wanaodaiwa kuwa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwa tuhuma za kupanga njama za uhalifu. Hata hivyo, CHADEMA kimejibu mapigo vikali, kikikanusha tuhuma hizo na kudai kuwa tukio hilo ni njama ya makusudi ya kutumia vyombo vya dola kukandamiza upinzani nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Kibaha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, alisema watuhumiwa hao walikamatwa Agosti 16, 2025, katika Ukumbi wa Mwitongo uliopo Mailimoja. Alisema polisi walipokea taarifa za kiintelijensia kuhusu kuwepo kwa mkutano wenye lengo la kupanga vitendo vya uhalifu na walifika eneo la tukio na kuwatia mbaroni watuhumiwa hao ambao wanaendelea kuhojiwa.
Kamanda Morcase aliwataja baadhi ya waliokamatwa kuwa ni Upendo Msechu, Upendo Mwalushwa, Pendo Mwasomola, Furaha Mbise, Kabuye Mzambia, na wengine wanne kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Hata hivyo, saa chache baada ya taarifa ya polisi, CHADEMA kilitoa taarifa rasmi kwa umma iliyotiwa saini na Mkurugenzi wake wa Mawasiliano, Brenda Rupia, ikipinga vikali madai hayo. Taarifa hiyo ilisema wanachama hao walikuwa kwenye kikao halali cha chama, kilichofuata katiba na sheria za nchi, na si kikao cha kihalifu.
"Tunauliza, kama kuna uhalifu unaweza kupangwa kwenye ukumbi wa hadhara, kwa nini usifanyike kwa siri? Polisi wanapataje taarifa za uhalifu kutoka kwenye vikao halali vya chama vilivyofanyika wazi?" ilihoji sehemu ya taarifa ya CHADEMA.
Chama hicho kimemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kuingilia kati na kuwaachia mara moja wanachama wao bila masharti. Aidha, kimetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na watetezi wa demokrasia kupaza sauti dhidi ya kile walichokiita "vitendo vya kubambikizia kesi wananchi" na jaribio la kuua demokrasia, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi. CHADEMA kimesisitiza kuwa hakitarudi nyuma wala kuogopa vitisho vya aina yoyote.