Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu, Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro limetoa uhakikisho kamili kwa wananchi kuhusu usalama, huku likifafanua kwamba uwepo wa askari na magari ya doria mitaani ni sehemu ya maandalizi ya tahadhari ya uchaguzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amesema wananchi hawapaswi kuwa na hofu au kuchukulia vibaya kuonekana kwa vyombo vya usalama mitaani, akisisitiza kuwa hii ni hatua ya kawaida inayochukuliwa katika kipindi cha uchaguzi ili kulinda amani.
"Wananchi wema hawapaswi kuogopa muonekano wa vyombo vyetu vya usalama, bali wachukue kama fursa ya kutimiza jambo hili la kikatiba (kupiga kura)," alisema SACP Mkama. Alihimiza kila raia kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
Aidha, Kamanda Mkama alisisitiza kwamba kila raia ana wajibu wa kulinda amani kwa kuepuka vitendo vya uchochezi, maandamano, na aina yoyote ya vurugu. Alionya kuwa uhujumu wa miundombinu ya uchaguzi, kufunga barabara, kujeruhi, au kufanya ghasia ya aina yoyote "itatatafsiriwa ni jaribio la kuvuruga amani," na hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
Baadhi ya wakazi wa Morogoro wameunga mkono hatua ya polisi. Rahma Kanika na Bright Dismas walipongeza hatua ya polisi kuimarisha doria, wakisema inatoa faraja na kuonesha serikali ipo makini kulinda usalama wa raia wake.
Hata hivyo, wananchi wengine, ikiwemo Juma Ismail na Anitha Peter, wameshauri askari wenye sare wasikae jirani kabisa na vituo vya kupigia kura, ili kuondoa hofu na kuhakikisha wananchi wanajisikia huru kutimiza haki yao ya kikatiba.